Serikali ya Tanzania inatarajia kunufaika kupitia ushirikiano na nchi ya Estonia katika masuala ya Tehama na Usalama Mtandao
ikiwemo kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya akili bandia (Al), teknolojia ya mifumo kuzungumza, usalama wa mitandao (cybersecurity), namba ya utambulisho ya kidijitali, ubalozi wa data, uhuru wa data, ukuaji wa biashara changa na uchumi wa kidijitali.
Kufuatia mazungumzo ya Ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Maryprisca Mahundi jijini Turti nchini Estonia na ule wa Estonia ulioongozwa na Dk Nele Leosk na Mali Liis Vahi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Estonia, nchi hizo zimekubaliana kushirikiana ili kubadilishana uzoefu na njia bora za kuboresha wananchi wa pande zote mbili..
Naibu Waziri Mahundi anashiriki Kongamano la 10 la Utawala wa Mtandao lenye kauli mbiu ya (Unlocking Digital Success) amesema nchi zote mbili zilijadili ushirikiano kati ya Estonia na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo na jinsi ya kukabiliana na changamoto za dunia katika maeneo ya akili mnemba, teknolojia ya mifumo ya kuzungumza, usalama wa mitandao, namba ya utambulisho ya kidijitali, (data-embassy) ukuaji wa taasisisi changa za ubunifu (startup growth) na masuala ya uchumi wa kidijitali.
Tanzania inashiriki katika Kongamano la 10 la Utawala wa Mtandao ambalo ni jukwaa muhimu la kujadili viwezeshi mbalimbali vya mapinduzi ya kidijitali duniani.
Kwa siku mbili za kongamano hilo, zaidi ya watu mia tano kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekusanyika, ikiwa ni pamoja na watoa maamuzi wa maendeleo ya mambo ya kidijitali, watunga sera, na wadau wa maendeleo kutoka Nchi 67 duniani na ushiriki wa Tanzania katika kongamano hili ni muhimu kwani unaimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya kidijitali duniani.