Kibaha. Watu 1,627 waliokutwa na ugonjwa wa vikope kwenye halmashauri tatu za Mkoa wa Pwani wameendelea kupata matibabu ili kuepuka upofu.
Idadi hiyo imebainika kufuatia utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya ikishirikiana na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Sightsavers yenye makao yake makuu nchini Uingereza.
Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani Dk Benedicto Ngaiza leo Mei,23,2024 wakati wa uzinduzi wa mradi wa kutokomeza ugonjwa huo wilayani Bagamoyo.
“Leo tunazindua mradi huu kwa hatua ya Halmashauri ya Bagamoyo na waathirika wataanza kupata matibabu ndani ya mwezi huu bila malipo,” amesema.
Ametaja chanzo cha kuenea ugonjwa huo ni uchafu wa mazingira na kutonawa mikono na kutoa wito kwa jamii kuzingatia suala la usafi.
Mkurugenzi wa Sightsavers inayojihusisha na kuzuia upofu unaozuilika na kutetea haki za watu wenye ulemavu, Godwin Kabalika amesema ili kufikia malengo kuna umuhimu wa jamii kuunga mkono juhudi hizo.
“Bagamoyo tutaanza mwezi huu wa tano hadi mwezi wa saba mwakani hapo tutakuwa tumefikia lengo, lakini ushirikiano kwa jamii ni muhimu hivyo tunaomba kuungwa mkono,” amesema.
Amesema kuwa ingawa ugonjwa huo ulianza miaka mingi nchini, lakini kadri siku zinavyokwenda jamii imeendelea kujisahau hali inayosababisha kuongezeka kwa tatizo hilo.
Amezitaja halmashauri zenye idadi kubwa ya wagonjwa kuwa ni Chalinze (804), Kibaha (435),na Bagamoyo (388).
Awali mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchata, amewataka wananchi wilayani humo kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa afya watakapoanza kutoa huduma hiyo ili kufikia malengo.
Veronika Mbena, mkazi wa Mkoa wa Pwani amesema kuwa ili kufikia malengo ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo, kuna umuhimu wa Serikali kuwekeza katika utoaji wa elimu kwa jamii ili itambue namna ya kujikinga.