Unguja. Ili kuimarisha miundombinu, kuinua kiwango cha elimu na kuondoa utaratibu wa mikondo miwili ya asubuhi na jioni, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imepanga kujenga madarasa 1,500 katika mwaka wa fedha 2024/25.
Pia, itaimarisha matumizi ya teknolojia ya kufundishia na kujifunzia kwa kuunganisha na mkongo wa Taifa wa mawasiliano na taasisi za elimu zikiwamo shule za sekondari 217, vituo vya walimu 12 na vituo vya ubunifu wa kisayansi 22. Pia, vitapatiwa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Hayo yamebainishwa na Waziri mwenye dhamana, Lela Muhamed Mussa alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo katika Baraza la Wawakilishi leo Mei 24, 2025 Chukwani, Zanzibar.
Wiziri Lela ametaja vipaumbele vingine vya wizara ni kujenga nyumba 20 za walimu, matundu ya vyoo 300, mabweni manane na kuyafanyia ukarabati mkubwa na mdogo na shule 100 za msingi na sekondari.
Amesema watajenga karakana za elimu ya amali katika shule 33 za sekondari Unguja na Pemba (karakana tatu kwa kila wilaya) na kujenga uzio katika shule za sekondari za Hasnuu Makame na Mohamed Juma Pindua.
Kipaumbele kingine katika bajeti hiyo ni kuendelea kutekeleza mtalaa mpya wa umahiri kwa elimu ya maandalizi, msingi na sekondari kwa kuwapatia walimu mafunzo na vifaa vya kujifunzia na kufundishia, vikiwamo vya watoto wenye mahitaji maalumu.
Amesema wataimarisha mafunzo ya ufundi na amali kwa kujenga vyuo vitano vya mafunzo ya amali, utanuzi wa Chuo cha Karume (KIST) na ujenzi wa chuo cha ubaharia, ambavyo pia vitapatiwa vifaa.
Waziri Lela amesema kipaumbele kingine ni kuimarisha elimu ya juu kwa kuongeza fursa ya upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu Zanzibar kuanzia ngazi ya diploma, pia kuanza mradi wa kujenga kampasi ya kudumu ya Chuo cha IIT Madrasa.
Serikali itajenga maabara ya sayansi ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), ujenzi wa shule ya afya, shule ya meno na kliniki yake chuoni hapo.
Katika mpango wake, wizara inakadiria kukusanya Sh1.140 bilioni ikiwa ni mapato kutoka katika vyanzo vyake vikuu.
Miongoni mwa vyanzo hivyo ni usajili wa shule za binafsi, malipo ya leseni za walimu, ada za usajili wa shule, ada za kiingilio kwa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha sita.
Vyanzo vingine ni ada za usajili wa wanafunzi wa shule binafsi wanaofanya mitihani ya Taifa na usajili wa vituo vya kufanyia mitihani.
Katika kuimarisha lishe shuleni, amesema wanafunzi 63,732 wa ngazi ya elimu ya maandalizi na 20,807 wa elimu msingi katika shule 42 za Serikali wanafaidika na huduma ya chakula kupitia mradi wa lishe, huku wizara ikitoa ruzuku kwa wanafunzi 63,732 wa ngazi ya elimu ya maandalizi na 324,460 wa elimu ya msingi katika shule za Serikali.
Waziri Lela amesema wanafunzi 391,398 sawa na asilimia 104.4 wameandikishwa katika ngazi ya elimu ya msingi, kati yao wanaume ni 197,301 sawa na asilimia 105.1 na wanawake ni 194,097 sawa na asilimia 103.7.
Wanafunzi 58,128 wapya wameandikishwa kuanza darasa la kwanza kwa mwaka 2024, kati yao 29,287 ni wavulana na 28,841 ni wasichana, kati ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza, wanafunzi 51,584 sawa na asilimia 88.7 wamepitia elimu ya maandalizi.
Waziri Lela amesema uwiano wa walimu kwa wanafunzi ngazi ya elimu ya maandalizi umepungua kutoka 32 mwaka 2023 hadi kufikia 29 mwaka 2024, na uwiano wa wanafunzi kwa darasa ngazi ya elimu maandalizi umepungua kutoka 53 mwaka 2023 hadi kufikia 52 mwaka 2024.
Amesema uwiano wa walimu kwa wanafunzi ngazi ya elimu msingi umepungua kutoka 45 mwaka 2023 hadi kufikia 42 mwaka 2024 na uwiano wa wanafunzi kwa darasa ngazi ya elimu msingi umepungua kutoka 62 mwaka 2023 hadi kufikia 60 mwaka 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii, ya Baraza la Wawakilishi, Sabiha Filfil Thani, amesema wanaitaka wizara kuhakikisha michezo inakuwa sehemu ya vipaumbele vyake ili kuimarisha sekta ya michezo nchini.
Pia, wameitaka wizara kuwa makini katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa kuwa uzoefu umeonyesha katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa shule bajeti ya 2023/24 kumejitokeza kuongeza gharama zaidi kinyume cha makubaliano ya awali, hivyo kuigharimu Serikali kutuia fedha nyingi za ziada.
“Kamati inaishauri wizara iwe na wataalamu katika ofisi ya mipango kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa mujibu wa thamani ya fedha,” amesema Thani.
Wakichangia hotuba hiyo ya bajeti, licha ya kuonyesha kuridhishwa na mipango ya wizara na mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu, wajumbe wa Baraza wametaka kasi zaidi iongezwe kwa kuwa elimu ni msingi mkuu wa kila mwananchi.
Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said amesema bado jitihada zinaendelea kufanyika kuondoa changamoto ya mikondo miwili shuleni jambo linaloondoa ufanisi kwa wanafunzi kwani wanapata muda mfupi wa kujifunza.
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, wizara inahitaji Sh830.9 bilioni kutekeleza mpango wa maendeleo ya sekta ya elimu kwa matumizi ya kazi za kawaida na miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha hizo, Sh618.400 bilioni ni kutoka SMZ na Sh212.555 bilioni kutoka kwa wahisani.
Kwa fedha za SMZ, Sh308.7 bilioni kwa ajili ya kazi za maendeleo na Sh309.6 bilioni ni matumizi ya kazi za kawaida yanayojumuisha Sh213.9 bilioni za mishahara na Sh45.4 bilioni ni matumizi mengineyo, na Sh50.2 bilioni ni kwa taasisi za wizara zinazopokea ruzuku.