Umuhimu wa tiba za dharura katika kuokoa maisha

Tanga. “Sitasahau. Nilitumwa shambani kuangua nazi, yalikuwa maamuzi mapesi tu, kwani nilinyanyuka na kubeba kikapu changu na kwenda kukwea mnazi, lakini kabla sijamaliza kuangua nilidondoka chini na kupoteza fahamu,” anasema Elly Kimodoa (23), mkazi wa kata ya Fungo, wilaya ya Muheza.

Anasema pengine familia yake isingemtuma kwenda kuangua nazi shambani, ajali hiyo asingekutana nayo na sasa angekuwa anaendelea na shughuli zake za bodaboda kama kawaida yake.

Kimodoa kwa sasa amelazwa katika Idara ya tiba na huduma za dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo akiendelea na matibabu.

Elly alianguka kutoka juu ya mnazi hadi chini Aprili 2, mwaka huu mchana, kisha kuvunjika mguu wa kushoto, hali inayomfanya apoteze fursa ya kujiingizia kipato kupitia ajira yake ya bodaboda.

Akiongea kwa hisia huku akiwa amekaa kitandani, Elly anasema, “Nilielezwa ndugu na jamaa walinichukua na kunikimbiza hospitali ya Teule iliyopo Muheza, lakini baada ya muda hali yangu ilibadilika na kupoteza fahamu na ndipo waliponileta hapa hospitali ya Bombo. Sijawahi kupanda mnazi, ile ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kukwea, ulikuwa mrefu sana na ndio umeniletea athari kwenye mguu huu unaouona hapa,” anasema.

Anabainisha kuwa pengine kusingekuwa na huduma ya dharura katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo, huenda angepoteza maisha. Mbali na kupata ajali hiyo, kijana huyo anaamini kuwa atapona na kuendelea na shughuli yake ya kuendesha bodaboda kwa sababu ni kazi inayomuingizia kipato.

Wakati Elly akieleza mkasa wake, Kirua Mswaki, mkazi wa Segera, anasema yeye ni mara ya tatu kutibiwa katika idara hiyo, akisumbuliwa na shinikizo la juu la damu.

“Pengine isingekuwepo huduma hii hapa, huenda ningekuwa na wakati mgumu wa kupata matibabu ninapozidiwa,” anasema na kuongeza;

“Mbali na mimi kutibiwa hapa, pia nilishamleta mtoto wangu alikuwa na tatizo la upumuaji na alikuwa na hali mbaya, lakini alivyoingizwa idara hii, alipatiwa huduma kwa haraka na kupona,” anasema.

Scholastica Mundu ni Muuguzi kiongozi wa idara hiyo ya dharura, anasema bado jamii haina uelewa wa kutosha kuhusiana na kwenda kupata huduma idara ya tiba na huduma za wagonjwa wa dharura.

“Niwashauri wananchi wapatapo mgonjwa aliyezidiwa au ajali wampeleke katika vitengo vya huduma ya dhararu ili kuokoa maisha,” anasema Mundu.

Mkuu wa Idara ya Tiba na huduma za magonjwa ya dharura (EMD) Hospitali ya Bombo, Dk Arafa Kachenje anasema kabla ya kuanzishwa idara hiyo, wagonjwa wengi walienda moja kwa moja kumuona daktari.

“Kuwepo kwa idara hii, kumesaidia kwa kiasi kikubwa watu kutopoteza maisha,” anasema Dk Kachenje, wakati wa ziara ya mafunzo kwa wanahabari kutembelea mradi wa huduma za dharura nchini unaofadhiliwa na mfuko wa Abbott Fund Tanzania, wakishirikiana na Wizara ya Afya.

Hata hivyo, mwaka 2019 idara yake iliyoanzishwa kwa ufadhili wa mfuko huo, kwa siku inapokea wagonjwa kati ya 60 hadi 80 kwa ajili ya kupatiwa huduma za dhararu.

Anasema kati ya wagonjwa wanaofika kuhudumiwa kwa siku, nusu ya wagonjwa hao ni wale ambao figo zimefeli, matatizo ya moyo, kisukari pamoja na shinikizo la juu la damu na kwamba hiyo inaonyesha kuwa bado jamii haina utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.

“Wengine wanaofuatia kwa kupata huduma katika idara hii ni wagonjwa wanaotokana na ajali mbalimbali za mvunjiko na moto, ikifuatiwa na wagonjwa wa upasuaji,” anasema Dk Kachenje

Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa Abbott Tanzania, Profesa Hendry Sawe, anasema mfuko huo umetoa Sh444.7 milioni kwa ajili ya ukarabati na usimikaji vifaa tiba katika jengo hilo la EMD Hospitali ya Bombo.

Akizungumzia uwekezaji huo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema majengo ya huduma za dharura (EMD) yameongezeka. Majengo 23 ya EMD yamejengwa kwa miaka mitatu katika hospitali maalumu, kanda na mikoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba.

Upande wa ngazi ya msingi, amesema ujenzi wa EMD 82 katika ngazi za Halmashauri unaendelea, ambapo EMD 66 zimekamilika na zinatoa huduma na nyingine 16 ziko kwenye hatua ya ukamilishaji.

Waziri Ummy anasema kwa kipindi cha miaka mitatu, majengo mahususi ya huduma za dharura na ajali 105 yameanzishwa kutoka EMD 7 zilizokuwepo mwaka 2020 na kufanikisha huduma kwa wagonjwa 262,260 walionufaika na huduma hiyo nchini na kufanikiwa kupunguza vifo na kuokoa maisha kati ya asilimia 40-50, kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu

Related Posts