Dodoma. Zaidi ya vijana 2,000 kutoka vyama vya siasa, asasi za kiraia na Serikali wanatarajiwa kushiriki mdahalo wa kitaifa wa vijana kutoa mapendekezo kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mdahalo huo utajadili masuala kadhaa ikiwemo utekelezaji wa ajenda za kundi hilo, ikiwa ni sehemu ya kuangalia utendaji katika miaka mitatu ya Rais Samia madarakani na mwelekeo wa Tanzania.
Kongamano hilo litakalofanyika Mei 25, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, limeandaliwa na Nusrat Hanje ambaye ni mbunge wa viti maalumu anayewakilisha kundi la vijana.
Akizungumza na Mwananchi leo, Hanje alisema ameitisha mjadala huo wa kitaifa, kwa sababu anataka kuona sauti za vijana zinaendelea kusikika kutoka kila pembe ya Tanzania na utahusisha makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa.
“Mdahalo huo utatoa nafasi kwa vyama vya siasa na Serikali kusikia vijana wanataka nini, ndiyo sababu mwisho wa mdahalo huu tutasoma maazimio ili Serikali na vyama vya siasa viyachukue kwa hatua zaidi,” alisema.
“Mwaka huu na mwaka 2025 ni uchaguzi, sasa hivi vyama vya siasa vinaandaa ilani, lakini tuna hofu kama vijana wanashirikishwa kikamilifu. Vyama na Serikali vinatambua nafasi ya vijana, vinabeba matumaini na matarajio yao kwenye Ilani zao za uchaguzi na kuwapa nafasi?” alihoji.
Alisema kupitia kongamano hilo wataibua mjadala kusaidia kundi la vijana kusonga mbele na wataweka historia ya kushiriki michakato ya kiuongozi katika Taifa.
“Kutakuwa na jopo la wazungumzaji wanaotoka katika makundi mbalimbali ya kijamii, asasi za kiraia zinazojihusisha na vijana, viongozi wa vyama vya siasa wanaotoka katika jumuiya na mabaraza ya vijana,” alisema Hanje ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).
Kwa mujibu wa Hanje, nguvu kubwa ya Taifa ni vijana katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo, lakini katika kushika uchumi bado linaonekana liko nyuma, hivyo katika mdahalo huo kutakuwepo na wawakilishi watendaji wa wizara za kisekta zinazohusika na masuala ya vijana.
“Watakuwepo wawakilishi watendaji kutoka sekta za mifugo na uvuvi, madini, nishati, kilimo, watakaotueleza katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia, mambo gani wameyafanya kwa ajili ya vijana na kuna mikakati gani,” alisema.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT- Wazalendo, Abdul Nondo alisema kongamano hilo ni fursa nzuri kwa vijana kwa kuwa linawashirikisha kutoka vyama vya siasa tofauti na asasi za kiraia.
Alisema litasaidia kupata mawazo yanayofikiriwa na kundi hilo.
“Kuna mambo yamefanyika ndani ya miaka mitatu yanayogusa vijana hasa katika sekta za kilimo, lakini siyo kwa kiwango kikubwa, hivyo tunapaswa kupaza sauti katika mdahalo ili Serikali itusikie,” alisema.