Viwanja 18,840 vyapangwa Songea na mradi wa LTIP

Takribani viwanja 18,840 vimepangwa katika vijiji 7 ambavyo ni Peramiho A, Nguvumoja, Peramiho B, Lundusi, Morogoro, Maposeni na Parangu ambapo lengo la awali lilikuwa ni utoaji wa hatimiliki 10,000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

Halmashauri ya Wilaya ya Songea imeweza kuzidi lengo lililopangwa kwa kuwa wananchi wameupokea mradi na kutambua umuhimu wa maeneo yao kutambuliwa, kupangwa, kupimwa na kumilikishwa kutapelekea kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi na kupelekea kuongeza usalama wa milki zao.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Bw. Wilman Kapenjama Ndile wakati wa kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) wilayani humo katika ukumbi wa Posta – Peramiho, tarehe 23 Mei 2024 Mkoani Ruvuma.

‘‘Tumefanikiwa kuvuka lengo lililopangwa kutokana na ushirikiano na elimu iliyotolewa kwa wananchi hivyo kila kiongozi aendelee kusimamia eneo lake ili kuhakikisha zoezi hili la urasimishaji linakamilika na wananchi kumilikishwa maeneo yao’’ alisema Ndile

 

Msimamizi wa Mradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea – Peramiho Bw. George Salu amesema kuwa mradi umeweza kuvuka lengo lake katika utekelezaji kwa kuwa wananchi wameonyesha utayari wa kushiriki shughuli mbalimbali za mradi, kuwepo kwa mpangilio mzuri wa makazi yenye nafasi katika baadhi ya vijiji, uwepo wa barabara za mitaa ambazo zinatumika kwa sasa, uwepo wa baadhi ya maeneo ya huduma za jamii kama shule, zahanati n.k na uwepo wa huduma za maji na umeme.

Akimwakilisha Meneja Mradi kwa upande wa Mjini Bw. Paul Kitosi amesema kuwa Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kupitia Wizara ya Ardhi katika utekelezaji wa Mradi huu imetoa kipaumbele kwa ushiriki wa sekta binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Mashirika ya Kijamii.

‘‘Takribani asilimia themanini (80%) ya kazi zote za urasimishaji mijini zitatekelezwa na Makampuni binafsi yaliyosajiliwa kufanya kazi za upangaji (mipango miji) na upimaji wa ardhi aidha asilimia (20%) ya kazi hizo zinatekelezwa na Serikali kupitia watumishi walioko katika Halmashauri husika’’ alisema Kitosi.

Wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Miliki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Nyumba Ardhi na Makazi kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa kueleza kuwa kwa kupata hatimiliki kutapelekea kuongezeka kwa usalama wa maeneo yao na kuwasaidia kujikomboa kiuchumi pindi watakapokuwa wanataka kupata mikopo benki.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unatekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika Halmashauri mbalimbali nchini ukiwa na lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kuzingatia haki za makundi maalum.

 

Related Posts