Wabunge wacharuka kukatika kwa umeme

TATIZO la kukatika kwa umeme kila mara katika maeneo mbalimbali ya nchi limewaamsha wabunge ambao kwa nyakati tofauti wameibana Serikali bungeni na kuitaka kueleza mikakati ya kumaliza changamoto hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yamejiri baada ya Mbunge wa Kilombero Abubakar Asenga (CCM) katika swali lake la msingi kuitaka Serikali ieleze lini itamaliza mgao wa umeme kwa siku za Jumanne na Alhamisi unaotokea katika jimbo lake.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega (CCM) alihoji lini tatizo hilo la kukatika kwa umeme litaisha katika mkoa wa Iringa, vivyo hivyo kwa Mbunge wa viti maalumu, Dk. Christine Ishengoma (CCM) alitaka kufahamu lini tatizo hilo litaisha katika Manispaa ya Morogoro.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kukatika kwa umeme katika jimbo la Kilombero kulisababishwa na ujenzi wa Barabara ya Ifakara – Kidatu.

“TANESCO ilikuwa na zoezi la kuhamisha nguzo za umeme zilizokuwa ndani ya Barabara. Lengo lilikuwa kuruhusu ujenzi wa barabara kufanyika na zoezi hilo limekamilika.

Abubakar Asenga

“Aidha, kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Ifakara kumepelekea kuimarika kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Jimbo la Kilombero,” amesema na kuongeza kufikia mwisho wa mwezi huu, itakuwa imempata mkandarasi atakayepewa zabuni ya kupeleka katika vijiji 15 vya jimbo hilo ambavyo havijpata umeme.

Kwa upande wa kukatika umeme katika mkoa wa Iringa na manispaa ya Morogoro, Kapinga aliendelea kusisitiza kuwa tatizo kubwa ni uchakavu wa miundombinu hivyo wizara hiyo inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha mindombinu hiyo ikiwemo kuongezea uwezo vituo vya kupoza umeme.

Malalamiko hayo ya wabunge yanajiri ikiwa imepita miezi kadhaa ya mgawo mkubwa wa umeme ambao umetamatika Machi mwaka huu baada ya baadhi ya mitambo ya Bwawa la Mwalimu Nyerere kuwashwa.

Related Posts