Dodoma. Wabunge wamecharuka kuhusu migogoro ya ardhi na ucheleweshaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha maeneo kwa ajili ya miradi.
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ametaja vifo na majeruhi waliotokana na fidia isiyo na masilahi kwa wananchi wanaopisha maeneo ya uchimbaji.
Wabunge wameeleza hayo wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2024/25. Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh171.37 bilioni.
Waitara amesema shida inatokea wakati wananchi wanapotakiwa kupisha maeneo yenye madini kulipwa Sh5 milioni, lakini kwenye maeneo yasiyo na madini fidia ni Sh30 milioni.
Amesema wawekezaji wanasema shida ni sheria za Tanzania, hali inayowafanya kubaini wanaowaumiza wananchi ni Serikali kupitia sheria.
“Leo nimesema nimuombe Mungu, nizungumze taratibu maana humu nimeshalia sijasikilizwa, nimerukaruka kichura sijasikilizwa, nimevua koti bado imekuwa ngumu nimeamua nizungumze kwa upole,” amesema.
Waitara amesema Mei 22 mwaka huu saa 7.00 mchana katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime, vijana waliungana kuvamia mgodi kitendo kilichosababisha mapambano dhidi yao na polisi, ambayo yalisababisha vijana wawili kufariki dunia akieleza wanazikwa leo (kesho).
“Kwa hiyo hali ya kisiasa ni tete kweli katika eneo lile, Mei Mosi binti Neema Omary (16) alipigwa risasi, nikaenda pale tukamtoa risasi mbili, mwaka huu, Aprili 26 ameuawa mtu, Mei 5 ameuawa mtu, Mei 22 wanne,” amesema.
Amesema chanzo cha migogoro hiyo kinasababishwa na utaratibu wa kufidia wananchi wanaokutwa na miradi kwenye maeneo yenye madini.
Waitara amesema mtu akilipwa Sh5 milioni na kuhama baadaye watoto wanapokuwa na kuonyeshwa maeneo ambayo yalikuwa yakimilikiwa na wazazi wao hutokea vurugu.
“Tuwe na mikataba ya ubia kwamba kama mtu akichukuliwa eneo lake lenye madini basi kuwe na ubia kati yake na mwekezaji,” amesema.
Amesema maeneo ya Nyamwaga mtathimini mkuu wa Serikali alifanya tathimini lakini baadaye ikaonekana gharama ya fidia ni kubwa hivyo watu hawajalipwa.
Amesema hali hiyo imefanya kila kiongozi anayefika maeneo hayo kuulizwa kuhusu fidia ya wakazi wa Komarera North. Alishauri Wizara ya Ardhi na Wizara ya Madini kuwasikiliza wananchi hao ili walio na haki walipwe.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda amesema ardhi ya wananchi imekuwa ikichukuliwa lakini kulipwa ni shughuli, akieleza wapo waliokaa miaka mitano bila kulipwa fidia.
“Hili linasononesha. Hivi leo niliposimama hapa, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma tayari kuna wananchi maeneo yao yamepimwa na wameambiwa wasiendeleze chochote, wasubiri fidia lakini sasa ni miezi saba fidia hawajapata,” amesema.
Amesema watu hawawezi kufanya ukarabati wakisubiri fidia ili waweze kuondoka.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Najma Giga amesema kuna ucheleweshaji fidia wakati Serikali au taasisi zake zinapotaka kutwaa maeneo ya wananchi kwa manufaa ya umma au kupangiwa matumizi mengine tofauti na yale yaliyopo kwa sasa.
“Ili kukadiria kiasi cha fidia kitakacholipwa kwa mwananchi ambaye mali zake zimetwaliwa kwa manufaa ya umma, sheria inaelekeza thamani ya mali hizo zinapaswa kukadiriwa na mthamini aliyesajiliwa na bodi ya wathamini,” amesema.
Amesema ucheleweshaji wa kulipa fidia unachangia kuzalisha migogoro kati ya wananchi na Serikali au mwekezaji, kulipa riba kutokana na kuchelewesha kulipia fidia, mlundikano wa kesi za ardhi katika mabaraza ya ardhi na mahakamani.
“Kamati inashauri Serikali ihakikishe kunakuwa na uthibitisho wa uwepo wa fedha za kulipa fidia ambao utatolewa na wizara au taasisi mtwaaji au mwekezaji anayekusudia kutwaa ardhi husika,” amesema.
Kamati ilisema Serikali ihakikishe kwa kushirikiana na wadau wote muhimu wa utwaaji, inafanya uhakiki kabla ya mthamini mkuu kuidhinisha majedwali ya fidia, na kabla ya hatua ya uonyeshaji majedwali hayo kwa wananchi kufanyika.
Amesema hiyo itasaidia kurekebisha dosari zote ndani ya muda sahihi na kuhakikisha wananchi wanalipwa kwa wakati.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema malalamiko ya fidia yanatokana na wananchi kutofahamu kwa hakika wadau wanaohusika na ulipaji wa fidia.
Amezitaja sababu nyingine ni baadhi ya taasisi kufanya uthamini wa fidia bila kuwepo fedha kwa ajili ya malipo, na kutozingatiwa kwa taratibu za uhakiki wa taarifa za uthamini wa fidia kwa mujibu wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, Sura 138.
Amesema ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara, wizara imetoa Waraka wa Uthamini na Fidia Na. 1 wa Mwaka 2024.
Amesema waraka huo pamoja na mambo mengine unaelekeza taratibu zinazopaswa kuzingatiwa wakati wa shughuli za uthamini, uhakiki wa taarifa za uthamini na ulipaji wa fidia.
“Naomba ifahamike kuwa, jukumu la wizara ni kuratibu uthamini na wajibu wa kulipa fidia ni wa taasisi itakayonufaika na uthamini huo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Silaa amesema Mfumo wa Usimamizi wa Huduma za Ardhi utaanza kufanya kazi Juni mwaka huu kwa awamu.
Amesema awamu ya kwanza ya mfumo itaanza kutumika Arusha, Tanga, Mbeya, Mwanza na Dodoma.
Silaa amesema mfumo huo utaondoa changamoto ya miliki pandikizi, hivyo kudhibiti migogoro ya ardhi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee amesema mwaka jana wizara ilisema kazi zitakazokamilika mwaka 2023/24 ni pamoja na kukamilika kwa mradi wa Kawe 711, lakini jana Silaa aliwaambia umefikia asilimia 35 na wanatarajia kukamilika mwaka 2026.
“Kwa nini mwaka jana mlilidanganya Bunge au Serikali hamjui au hamna mipango, mnafanya kwa kubahatisha,” amehoji Mdee.