Wakulima Kising’a walia kukosa intaneti

Iringa. Kama hujafanya mawasiliano ikiwamo kuaga ndugu, jamaa na marafiki kabla ya kufika Kijiji cha Kising’a wilayani Kilolo, ujue ukifika huko simu yako haitakuwa na kazi.

Jambo hili ndilo linalowafanya wakulima kulia kwa kukosekana mitandao wa intaneti jambo linalowafanya waone kama wanaishi kisiwani wakiwa hawajui mabadiliko ya bei za mazao baada ya mavuno.

Kising’a wanalima matunda kama parachichi, mbogamboga, mahindi, maharagwe na mazao ya misitu kwa ajili ya mbao, nguzo za umeme na bidhaa nyingine.

Wakizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Mei 23, 2024, wananchi hao wamesema wanapata mtandao wa intaneti mmoja ambao pia kiwango chake kipo chini na wakati mwingi unakatika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kising’a, Wilson Lulenga amesema kukosekana kwa mawasiliano hayo kumewafanya wabaki kuwa maskini licha kuwa na mazao mengi huku miundombinu yote ikiwepo.

“Tunao umeme, barabara ni nzuri na mazao yanastawi lakini huwezi kuingia mtandaoni ukaperuzi kujua wapi soko lipo juu na wapi hakuna soko, baada ya mavuno huwa tunashtuka walanguzi wamekuja kijijini na bei zao basi tunauza,” amesema Lulenga.

“Tunaomba watuletee mitandao. Mtu unalima halafu ukienda sokoni ndio unashtuka kumbe bei iliporomoka,” amesema.

Eneo la Kijiji cha Kising’a, wilayani Kilolo ambalo lina changamoto ya mtandao hasa intaneti.

Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Kising’a, Herode Kisoma amesema simu yake kubwa anayomiliki imekuwa kama pambo kwa sababu ili aweze kuperuzi lazima apandishe mlimani au ajitege sehemu.

“Kuna mahali ukisimama ndio walau unapata mtandao lakini maeneo mengine hakuna kitu. Ukitaka kutuma taarifa basi uende ukajitege sehemu, hii ni mbaya kwetu,” amesema na kuongeza;

“Tunaomba kuletewa mtandao sio huu wa 2G unaopatikana kwa kusuasua, watuletee hata 3G,” amesema Herode.

Mmoja wa wakulima wa Kising’a, Adam Mwilafi amesema ikiwa wataanza kupata huduma za mawasiliano, hali ya maisha yao itabadilika kuliko hivi sasa ambapo wanaishi kama kisiwani.

Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga amesema maombi ya wananchi hao ameshawasilisha bungeni mara kadhaa na kwamba anatarajia katika mgao wa minara ya simu, eneo hilo litakumbukwa.

“Ni kweli hali ya mawasiliano kule ni ngumu na wanazalisha mazao mengi, naweza kusema hakuna matunda ambayo hayastawi kule. Wanapata mvua za kutosha karibu mwaka mzima shida ni hayo mawasiliano,” amesema Nyamoga.

Related Posts