Wanafunzi Sekondari ya Sangu waandamana, wapinga mkuu wa shule kuhamishwa

Mbeya. Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Sangu ya jijini Mbeya wamesema wapo tayari kuondoka shuleni hapo, kama Mkuu wa shule hiyo, Jacob Msigwa atahamishwa kama walivyosikia.

Leo Ijumaa Mei 24, wanafunzi hao wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti, wameandamana shuleni hapo wakipinga hatua hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, baadhi ya wanafunzi hao wamesema hawakubaliani na taarifa zilizosambazwa shuleni hapo za kuhamishwa kwa mwalimu huyo, wakidai ameibadili kwa kiwango kikubwa, kumuondoa ni kutaka kurudisha nyuma maendeleo ya shule hiyo.

Akizungumzia hilo, rais wa serikali ya wanafunzi shuleni hapo, Emanuel Joshua amesema wameamua kuungana wanafunzi kupinga hatua hiyo baada ya tetesi walizopata jana usiku kwamba mkuu huyo  anahamishwa.

Amesema tangu alipohamia shuleni hapo  mapema mwaka jana, Mwalimu Joshua amefanya mabadiliko makubwa kitaaluma, usafi na nidhamu kwa wanafunzi ambayo iliporomoka kutokana na usimamizi mbovu.

“Kitaaluma ameibadilisha shule, mwaka juzi kulikuwapo na ziro kibao hapa, lakini mwaka jana alipoanza tumepata one ya saba kidato cha nne, tunakubalije aondoke!” amesema rais huyo.

Naye Leonia Mbilinyi, amesema wapo tayari kuondoka shuleni hapo iwapo watamhamisha mwalimu huyo.

“Taaluma, majengo, nidhamu na motisha za mara kwa mara kwa wanafunzi baada ya mitihani, imetuhamasisha sana kupenda shule, wanapotaka kumhamisha lazima wafikirie mara mbili.Huyu kaibadili shule ndani ya muda mfupi, Sangu ilikuwa inafanya vibaya sana kwenye mitihani ya Taifa, lakini miaka hii miwili imebadilika sana, akiondoka na sisi tutahama,” amesema Leonia anayesoma kidato cha tano.

Naye makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi,  Lydia Mwampashi ,amesema wamepokea kwa mshtuko taarifa za kuhamishwa kwa mwalimu huyo.Anasema wanafunzi kwa umoja wao wanapinga hatua hiyo.

“Mtu anayekupa maendeleo ndani ya muda mfupi, wakati huohuo unaona mpango kazi wake ni wa muda mrefu unamhamishaje, hatukatai mwalimu kuhama kutoka shule moja kwenda nyingine, lakini hii shule iliharibika ameirudisha kwenye mstari ndani ya muda mrefu, wamuache kwanza ajenge msingi imara tusije tukarudi kule tulikotoka,” amesema Lydia.

Akizungumza shuleni hapo, Msigwa anasema hakuwa na taarifa yoyote ya uamuzi wa wanafunzi wake na wala hajui kinachoendelea, ameshtushwa na maandamano hayo.

Hata hivyo, amesema: “Mimi ni mtumishi, nafanya kazi popote nitakapopangiwa kufanya kazi.”

Amesema pamoja na taharuki iliyojitokeza leo shuleni hapo, amewaomba wanafunzi kuwa watulivu kwa kuwa taarifa hizo hazina ukweli.

“Maandamano yao yamenishtua sijui wamechukua wapi hizi taarifa, zimezua taharuki na zimewaharibu kisaikolojia na kitaaluma, sijapewa taarifa yoyote kuhusu kuhamishwa, mimi ni mtumishi popote nafanya kazi,” amesema Msigwa.

Hata hivyo, amesema baada ya habari za maandamano kusambaa, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao ni wamiliki wa shule ngazi ya mkoa na maofisa elimu walifika shuleni hapa haraka na tayari wametatua mtanziko huo.

“Tayari wanafunzi wamesharejea madarasani kuendelea na masomo,” amesema Msigwa.

Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya, Abdul Komba amesema suala hilo kwa sasa limefikishwa kwa mamlaka za juu watalifanyia kazi.

“Suala hili limetushtua, tayari tumelifikisha ngazi za juu kwa Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi ambaye atalitolea ufafanuzi,” amesema kiongozi huyo.

Related Posts