Dar es Salaam. Uongozi bora, taasisi imara na uwezeshaji wananchi kiuchumi, ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa msingi wa ulinzi wa amani na usalama wa Afrika.
Sambamba na mambo hayo kwa mujibu wa wabobezi wa diplomasia, ushirikishwaji wa vijana katika ulinzi wa amani, ni jambo lingine muhimu kwa usalama wa bara hili.
Licha ya mitazamo hiyo kuhusu amani ya Afrika, wanadiplomasia hao wameonya wingi wa wahitimu wa elimu ya juu pasina ajira kuwa ni hatari mpya kwa usalama wa Afrika.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo, Ijumaa Mei 24, 2024 katika mhadhara uliozungumzia ‘Ulinzi na Amani inayotakiwa Afrika’ ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Katika wasilisho lake, Mhadhiri wa Masomo ya Kimkakati katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Profesa Eginald Mihanjo amesema ulinzi na amani vinashabihiana na uwezo wa kiuchumi wa wananchi.
Ameijenga hoja hiyo kwa maelezo kuwa, msingi wa uchumi ni wananchi hasa vijana baada ya kuhitimu elimu ya juu wawe kwenye ajira.
Kinyume na hivyo, amesema ni vigumu nchi husika kuwa na amani kwa kuwa vijana wengi hawana cha kufanya.
“Kwa sasa Afrika ina idadi kubwa ya wahitimu wa shahada wasio na ajira, ni vigumu kuwa na amani katika mazingira hayo.
“Kufikia mwaka 2050 zaidi ya asilimia 50 ya watu wa Afrika watakuwa vijana na inawezekanaje kuwa na amani iwapo wanataka kuingia kusaka fedha na hawana ajira?,” amehoji.
Mtazamo huo, unashabihiana na alichokiwasilisha Mhadhiri wa Uhusiano wa Kimataifa, Profesa Adebayo Ulukoshi, aliyesema ugumu wa amani ya Afrika unasababishwa na kukosekana kwa ajira.
Ameeleza kuwa hali ngumu ya kulinda amani katika mazingira ya umasikini.
Profesa Adebayo amesema mataifa mengi ya Afrika yana vijana wengi, lakini asilimia kubwa hawana ajira.
“Amani haiwekezwi kwa kuwa na vikosi vingi vya ulinzi na usalama au makombora, bali inahitaji kuwezesha wananchi ulionao kiuchumi,” amesema.
Kadhalika, ameeleza ugumu wa amani katika Bara la Afrika, unatokana na kuendelea kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.
“Hilo limeshuhudiwa katika machafuko ya nchini Sudan, wanawake wanatekwa, wanabakwa na kufanyiwa kila aina ya ukatili,” ameeleza.
Wakati wa wasilisho lake, Profesa Mihanjo amesema ombwe la uongozi bora ni sababu nyingine ya kuvurugika kwa amani Afrika.
Hoja hiyo ya Profesa Mihanjo ilitokana na swali lililoulizwa mwanadiplomasia mbobezi, Balozi Liberatha Mulamula aliyetaka kujua sababu za kuendelea kwa machafuko Jamhuri ya Demokrasi aya Congo, licha ya juhudi zinazofanyika kuyasitisha.
Profesa Mihanjo amesema kuendelea kwa hali ngumu ya amani katika nchi za Afrika, ni matokeo ya uongozi mbaya.
“Tutafichaficha lakini ukweli ni kwamba kuna ombwe la uongozi linalosababisha haya mambo yaendelee,” amesema.
Kuhusu hilo, Profesa Adebayo amesema msingi wa amani na usalama inayotakiwa Afrika ni kuwa na viongozi bora.
Viongozi bora kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, hawatakuwa sababu ya ugomvi wa wananchi na watasimamia maslahi ya Afrika.
“Nani anapaswa kuwa kiongozi, nani anapaswa kushauri, nani anapaswa kuwa mfano wa amani Afrika lakini tuwe na taasisi imara hapo tutakuwa na amani tunayoitaka Afrika,” amesema.
Kamishna wa Masuala ya Kisiasa, Ulinzi na Usalama wa Umoja wa Afrika (AU), Balozi Bankole Adeoye, amesema kuna haja Baraza la Usalama la Afrika kuwashirikisha vijana.
Amesema amani inayotakiwa Afrika ni ile itakayowezesha vijana na wanawake kuwezeshwa kwa kila namna.
Amani hiyo, amesema itajengwa kwa kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto Afrika.
Balozi mstaafu Paul Mella, amesema kwa sasa mahitaji vya ulinzi wa usalama yanaongezeka kwa kuwa machafuko ya nchi moja na nyingine yanaongezeka pia.
Lakini, amesema changamoto kubwa ni maeneo mengi wanakotumwa walinzi wa amani huwa ni makubwa kuliko vikosi vinavyotumwa.
Amesema katika baadhi ya nchi, pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa, kuna changamoto ya kuyafikia maeneo mbalimbali.