Waziri Slaa aeleza hatima nyumba za miradi ya NHC

Dodoma. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeliomba Bunge kuwaidhinishia Sh171.37 bilioni huku ikisema ujenzi wa mradi wa Kawe 711 utakamilika mwaka 2026.

Waziri Jerry Silaa leo Mei 24, 2024 amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25 na kusema mwaka 2023/2024 Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), lilipanga kukamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ikiwemo mradi wa nyumba 422 wa Kawe 711 wenye thamani ya Sh169 bilioni.

Amesema pia walipanga kujenga nyumba 196 katika mradi wa  Golden Premier Residence wenye thamani ya Sh71 bilioni. Bila kutaja sababu, Silaa amesema miradi hiyo ilikuwa imesimama tangu mwaka 2018.

“Ujenzi wa mradi wa Kawe 711 unaendelea na umefikia asilimia 35 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026,” amesema na kuongeza kuwa mradi wa Golden Premier Residence (GPR) bado umesimama na majadiliano kati ya shirika na mkandarasi yanaendelea.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025, jijini Dodoma leo Mei 24, 2024. Picha na Edwin Mjwahuzi

Silaa amesema shirika limeendelea na uuzaji na upangishaji wa majengo katika mradi uliokamilika wa Morocco Square, ambapo katika jengo lenye nyumba za makazi 100 na kuwa tayari nyumba 71 zimeshauzwa na mauzo ya nyumba zilizobakia yanaendelea.

Aidha, amesema upangishaji wa hoteli yenye vyumba 81 umefanyika kwa asilimia 100, maduka asilimia 94 na ofisi asilimia 42.

Silaa amesema katika mwaka 2024/25, Serikali itaendelea na ujenzi wa nyumba 422 katika mradi wa Kawe 711 ambapo unatarajiwa kufikia asilimia 75 ya utekelezaji ifikapo Juni, 2025.

Amesema pia wataendelea na ujenzi wa nyumba 196 katika mradi wa Golden Premier Residence (GPR) ifikapo Juni, 2025.

Aidha, amesema wataanza ujenzi wa nyumba 560 za Mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) awamu ya pili katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam huku ujenzi wa nyumba 150 za Samia Housing Scheme katika eneo la Medeli na Iyumbu jijini Dodoma ukiendelea.

Related Posts