‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai ametetea nafasi yake baada ya kuzoa kura 45 dhidi ya kura 34 ambazo mpinzani wake, Emmanuel Chengule amepata. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mungai ameshinda uchaguzi huo uliofanyika jana Ijumaa mjini Iringa katika Kikao cha Baraza la Mashauriano Mkoa wa Iringa kilichoketi na kuwachagua viongozi wa mkoa huo watakaoongoza kwa miaka mitano ijayo.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi huo John Mrema amesema kila mgombea alipata haki ya kujieleza na kuchaguliwa.

Katika ngazi ya ukatibu, Leonard Kwirijira ameshindwa kwa kupata kura 46 wakati David Mfugwa amepata kura 35.
Kwa upande wa Bawacha, Susan Mgonokulima amepata kura 15 wakati mshindani wake Hamida Tanda akipata kura 14.

Itakumbukwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema – Bara, Tundu Lissu alikiambia kikao cha Kamati Kuu (CC) iliyoketi hivi karibuni kuwa madai ya rushwa alielezwa na Mungai.

Lissu ambaye almanusura akipasue chama hicho kwa tuhuma hizo za rushwa kwenye chaguzi za chama hicho, alikiambia kikao hicho, kwamba alifikia hatua ya kutoa kauli hiyo hadharani, baada ya kulalamikiwa kuwapo kwa rushwa kwenye chaguzi za chama chake na Mungai aliyekuwa anatetea nafasi yake kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo, Lissu akiwa kwenye kikao cha kamati hiyo ya Chadema, alijitetea kuwa kauli yake haikulenga kukidhoofisha chama hicho, bali kukiimarisha, ili wale wanaoendelea kutoa fedha hizo, kuacha kufanya hivyo, huku baadhi ya wajumbe wakisisitiza alichokifanya hakikuwa sahihi.

Related Posts