China yakamilisha luteka zake za kijeshi karibu na Taiwan – DW – 25.05.2024

Mazoezi hayo yalizinduliwa siku tatu baada ya Rais wa Taiwan Lai Ching-te kuchukua madaraka na kutoa hotuba ya kuapishwa ambayo China iliishutumu kama “tangazo la uhuru”.

Jumla ya ndege 111 za China na dazeni za meli za wanamaji zilishiriki katika mazoezi karibu na kisiwa hicho cha kidemokrasia, kulingana na wizara ya ulinzi ya Taiwan.

Jeshi la China “limekamilisha kwa mafanikio” operesheni hiyo, iliyopewa jina la “Joint Sword-2024A”, mtangazaji wa kituo cha habari cha jeshi kinachoendeshwa na serikali, CCTV-7 alisema katika matangazo Ijuma jioni.

Soma pia: China yaonya juu ya vita vya Taiwan baada ya luteka za kijeshi

Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wa China wameliambia shirika la habari la serikali Xinhua kwamba meli za Jeshi la Ukombozi wa Watu (PLA) zimeingia “karibu zaidi kuliko hapo awali” kwenye ufuo wa Taiwan.

Mazoezi hayo yalihusisha luteka za mashambulizi yanayolenga viongozi wa kisiwa hicho pamoja na bandari zake na viwanja vya ndege, walisema.

China, Beijing | Ripoti kuhusu luteka za za China karibu na Taiwan
Gari la kubeba vifurushi likipita mbele ya skrini inayoonyesha picha za habari za mazoezi ya kijeshi katika maeneo karibu na kisiwa cha Taiwan.Picha: Tingshu Wang/REUTERS

Hii “itakata ‘mishipa ya damu’ ya kisiwa hicho na kuzuia ‘ugavi wake wa misaada ya kigeni'”, Tong Zhen, mtaalam kutoka Chuo cha Sayansi ya Kijeshi, alinukuliwa akisema.

Mazoezi hayo yalilenga kupima “uwezo wa ukamataji wa pamoja na madaraka, mashambulizi ya pamoja na udhibiti wa maeneo muhimu”, Li Xi, msemaji wa Kamandi ya Mashariki ya PLA, alisema Ijumaa.

Mazoezi hayo ni sehemu ya kampeni inayoongezeka ya vitisho vya China ambayo imeshuhudia taifa hilo likifanya mfululizo wa mazoezi makubwa ya kijeshi karibu na Taiwan katika miaka ya hivi karibuni.

Azma ya China kuiunganisha Taiwan na bara

Taiwan imejitawala tangu mwaka wa 1949, wakati wazalendo walipokimbilia kisiwani humo kufuatia kushindwa na Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) katika vita vya wenyewe kwa wenyewe bara.

Beijing inakichukulia kisiwa hicho cha kidemokrasia kuwa sehemu ya eneo lake na haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu kukileta chini ya udhibiti wake.

Soma pia:Taiwan yasema ´vitimbi´ vya jeshi la China vimeongezeka 

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Beijing Wu Qian alisema Ijumaa kwamba Lai “amepinga vikali kanuni ya China moja… na kuwasukuma wenzetu wa Taiwan katika hali ya vita na hatari”.

Taiwani | Ndege za Jeshi la Anga la Taiwan F-16 zikiruka wakati wa safari ya doria
Ndege za Kikosi cha anga cha Taiwan chapa F-16 zikifanya doria katika eneo lisilojulikana nchini Taiwan katika picha hii iliyopigwa tarehe 23 Mei 2024, na kutolewa Mei 24, 2024.Picha: Taiwan Defence Ministry/Handout/REUTERS

“Kila tunapochokozwa na ‘uhuru wa Taiwan’, tutasukuma hatua zetu za kujibu hatua moja mbele, hadi tutakapokamilisha uunganishaji kamili wa nchi mama,” alisema.

Mzozo huo kwa muda mrefu umeufanya Ujia wa Bahari ya Taiwan kuwa miongoni mwa maeneo hatari zaidi duniani, na matukio ya wiki hii yamezua hofu kuwa China inaweza kutumia nguvu za kijeshi kukiweka kisiwa hicho chini ya utawala wake wa bara. Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zote kuepuka kuuchochea mzozo baina yao.

Marekani, mshirika mkubwa wa Taiwan na mfadhili wa kijeshi, iliihimiza kwa nguvu China siku ya  Alhamisi China kuchukua hatua kwa kujizuia.

Wizata ya Ulinzi ya Marekani Pentagon ilitangaza Ijumaa kwamba Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin atakutana na mwenzake wa China Dong Jun mwishoni mwa mwezi huu katika Mkutano wa Majadiliano wa Shangri-La, mkutano wa kila mwaka wa maafisa wa ulinzi kutoka kote ulimwenguni.

Chanzo: AFPE

Related Posts