Wakati mashabiki wa Yanga wakiendelea kufurika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, juu angani kuna burudani ya aina yake inaendelea.
Nje ya uwanja, kuna mistari na mashabiki wanaingia uwanjani na wengine wakiwa ndani tayari, lakini ile chopa ya Yanga nayo imekatiza hapa uwanjani na kuibua shangwe.
Chopa hiyo imezunguka mara mbili mbili juu ya eneo la Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa imepambwa kwa mabango ya ubingwa na mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Bara, Benki ya NBC.
Wakati chopa hiyo ikizunguka, ikasindikizwa na shangwe la mashabiki wa ndani na nje ya uwanja.
Chopa hiyo ni moja ya shamrashamra za kukabidhiwa kombe la ubingwa kwa Yanga, ambapo inaelezwa ndio itakayolishusha kombe hilo la ubingwa wa tatu mfululizo wa mabingwa hao wa soka, Tanzania Bara.
Yanga leo inacheza mechi yake ya 29 msimu huu dhidi ya Tabora United, ikiwa tayari na ubingwa mechi ambayo itatumika kuwakabidhi ubingwa wao huo wa 30 kihistoria.