Chopa yashusha Kombe kwa Mkapa

HATIMAYE ile chopa maalumu iliyokuwa na jukumu la kulileta Kombe la Ligi Kuu Bara litakalokabidhiwa Yanga mara baada ya mechi dhidi ya Tabora United, imelishusha kombe hilo huku mashabiki wakiisindikiza kwa shangwe kubwa.

Saa 8:48 mchana chopa hiyo imeshuka katikati ya eneo la kucheza la Uwanja wa Benjamin Mkapa kisha likashushwa kombe hilo la ubingwa la Yanga likiteremshwa na mrembo mmoja akisindikizwa na maafisa wa NBC ambao ndio wadhamini wa ligi.
 
Awali, kabla ya chopa hiyo kushuka ikazunguka juu ya uwanja huo kwa mara tatu kisha baadaye kushuka taratibu katikati ya uwanja huo.

Wakati wote ikizunguka mpaka kutua mashabiki maelfu wa Yanga waliokuwa majukwaani walikuwa wakishangilia kwa nguvu kufurahia tukio hilo linaloenda sambamba na Pati la Kibingwa Kwa Mkapa.

Baada ya kombe hilo kushuka dakika tatu baadaye chopa hiyo ikiruka na kuondoka uwanjani hapo huku taji hilo likiingizwa ndani.

Hii inakuwa mara ya kwanza kwa tukio la namna hiyo kwa kombe kushushwa na chopa ambapo Yanga inachukua taji lake la tatu la ligi mfululizo, likiwa ni taji la 30 kwa klabu hiyo tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965 ikiwa ndio kinara ikifuatiwa na Simba yenye mataji 22 kwa sasa, huku Mtibwa Sugar iliyopo katika janga la kushuka daraja ikishika nafasi ya tatu kwa kutwaa mara mbili 1999 na 2000.

Yanga itacheza mechi ya 29 ya Ligi Kuu kwa msimu huu kuanzia saa 10:00 jioni ya leo dhidi ya Tabora United na mara baada ya mchezo huo utakapomalizika ndipo klabu hiyo itapewa kombe hilo.

Related Posts