Coastal Union yakata tiketi CAF

WAGOSI wa Kaya, Coastal Union wamejihakikisha nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao baada ya leo kukata tiketi ya CAF kwa kutoka suluhu na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, kwani sasa imefikisha pointi 42 ambazo haziwezi kufikiwa na KMC iliyokuwa ikiifukuzia iliyo na pointi 36 na hata kama zitashinda mechi za mwisho zitafikisha 39.

KMC ilikuwa na uwezo wa kuzifikia pointi hizo 42, lakini kipigo cha leo kutoka kwa Simba kimeitibulia na kuiacha ibaki katika nafasi ya nne.

Matokeo ya KMC yameirahisishia Coastal kukata tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao sambamba na vigogo, Simba, Yanga na Azam. 

Mara ya mwisho kwa Coastal kushiriki michuano ya kimataifa ilikuwa mwaka 1989 iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika na kuishia raundi ya kwanza. Michuano hiyo ilikuja kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004.

Coastal inakuwa timu ya sita kukata tiketi ya CAF ikiwa nafasi ya nne baada ya KMC, Namungo, Biashara United, Geita Gold na Singida Fountain Gate, kutokana na Tanzania kupewa nafasi ya timu nne katika michuano hiyo, mbili zikicheza Ligi ya Mabingwa na nyingine Kombe la Shirikisho.

Yanga ndio bingwa wa Ligi Kuu na ipo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) linalotoa mwakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na Azam iliyopo nafasi ya pili katika Ligi Kuu, huku Simba ikiwa ya tatu na Coastal ikiwa ya nne.

Kama Yanga ingeingia fainali ya CAF na timu nyingine nje ya hizo mbili zilizopo nyuma yake na timu hiyo kubeba, Wagosi wasingekuwa na nafasi, kwani bingwa wa Ligi na mshindi wa pili wangekata tiketi ya Ligi ya Mabingwa na bingwa wa FA na mshindi wa tatu wa Ligi Kuu wangeenda Kombe la Shirikisho Afrika.

Related Posts