DC ahimiza matumizi ya pedi yazingatie uhifadhi wa mazingira

Arusha. Mkuu wa wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amewataka wadau wa hedhi salama, kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya taulo za kike (pedi) kwa kuzingatia usafi, uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Amesema kuwa baadhi ya taulo za kike hasa zinazotumika kutupa zimekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.

Mtahengerwa ameyasema hayo leo Mei 25, 2024 katika viwanja vya Makumbusho jijini hapa, ikiwa ni maadhimisho ya kitaifa ya siku ya hedhi duniani inayokwenda sambamba na upimaji wa afya ya uzazi.

 Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya, amesema kuwa hivi karibuni kumekuwepo na uchafuzi wa mazingira unaotakana na taka za pedi zilizotumika na kutupwa hovyo mitaani.

 “Vifaa hivyo vya kujisitiria siyo kitu kigeni lakini haileti  picha nzuri kukutana nazo mitaani, na nyie wenyewe ni mashahidi kila ukipita unakuta zimetupwa hovyo,”amesema Mtahengerwa na kuongeza;

“Hii si jambo zuri , kwa hiyo kadri tunavyoelekea mbele inaweza kusababisha hatari, hivyo tujitahidi kukabiliana na hilo mapema kwa matumizi yanayozingatia usafi na uhifadhi wa mazingira au kuja na vifaa rafiki wa mazingira” amesema.

Mtahengerwa ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa shule na taasisi za elimu ya juu  kuhakikisha wanawatengea wanafunzi wao wa kike chumba maalumu cha kujistiri anapokumbwa na hali hiyo ghafla.

“Wataalamu wasema unaweza kujua itatokea lini lakini huwezi kuipangia, hivyo kuna wakati mzunguko unavurugika na msichana kujikuta amekutwa na hali hiyo akiwa shule, tengeni vyumba vya  kujistiri kwao ili kutunza hadhi za watoto wetu lakini pia wasipoteze muda wao wa masomo” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa hedhi salama kitaifa, Dk Mariam Mashimba amesema kuwa miundombinu rafiki ya kujistiri kwa wasichana wanapokuwa katika siku za hedhi ni changamoto katika taasisi nyingi za elimu.

“Tumeshatoa maelekezo kupitia Wizara ya Elimu kila shule iwe na chumba cha kujistiri mwanafunzi anapokuwa katika siku zake ikiwa na maji safi ya kujisafisha kama amechafuka, iwe na pedi na pia mashine ya kuchomea taka hizo, ili kuepuka kukatisha masomo kwa siku atakazokuwa anapitia hali hiyo.”

Mbali na hilo amesema kwa sasa wanahamasisha zaidi matumizi ya taulo za kike zenye uwezo wa kutumika zaidi ya mara moja kwa kufua na kukausha kisha kutumika tena, ili kuepuka uchafuzi  wa mazingira lakini pia kusaidia uchumi wa baadhi ya jamii wasioweza kumudu kununua mara kwa mara.

Katibu wa jukwaa la hedhi salama nchini, Dk. Severine Alute amesema  kwa sasa wanaelimisha jamii juu matumizi sahihi ya pedi na madhara wanayoweza kukumbana nayo wakikiuka.

“Matumizi yasiyo sahihi  ya pedi yanaweza kusababisha matatizo kwenye uke na njia ya mkojo inayoletwa na bakteria hivyo katika kuepuka hili, tunatoa elimu ya matumizi sahihi ikiwemo kutumia pedi iliyothibitishwa na mamlaka za dawa na tiba, lakini pia kwa zile za kufua zitakate kisha zianikwe zikauke vema kwa ajili ya matumizi mengine,”amesema Dk Alute.

Mratibu wa  Matembezi ya hedhi salama, Japhet Jackson amesema lengo ni kuhakikisha jamii inafikiwa na elimu ya hedhi salama kupitia mazoezi lakini pia kutambua umuhimu wake kiafya na kiuchumi, hasa katika kuepuka maambukizi ya bakteria wanaoweza kusababishwa na hedhi isiyo salama ikiwemo uchafu katika siku hizo.

Related Posts