DC Kaganda aagiza wafanyabiashara Ngaramtoni kufungiwa maduka yao

Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha DC kuwafungia maduka wafanyabiashara wa eneo la Ngaramtoni hadi watakapofanya usafi kwenye mitaro iliyo karibu na maduka yao.

Mbali na hilo, amemtaka pia mkurugenzi huyo kuwapiga faini wafanyabiashara wote wa eneo hilo kwa mujibu wa sheria ya utunzaji wa mazingira, kwa kukacha kufanya usafi ili liwe fundisho kwa wengine, pia kwa usalama wa afya za watumiaji wa bidhaa zao.

 Kaganda ameyasema hayo leo Jumamosi, Mei 25, 2024 baada ya kuhitimisha kazi ya kufanya  usafi katika mji mdogo wa Ngaramtoni, Kata ya Olmotonyi.

Kaganda amesema kazi ya kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni ya lazima, lakini wapo baadhi ya wafanyabiashara na wananchi wanakiuka maelekezo hayo na kutegea utekelezaji wake.

“Mfano leo hapa nimekuja kuungana na wananchi wa eneo hili nikiwa na kamati nzima ya ulinzi na usalama, lakini hakuna mfanyabiashara hata mmoja amejitokeza kuungana na sisi kufanya usafi zaidi ya wananchi, wakati wao ndio wachafuzi wakubwa wa mazingira,” amesema Kaganda.

Amesema katika kazi hiyo, wamekuta baadhi ya mitaro imeziba kwa taka hasa za chupa za plastiki zinazosababishwa na matumizi ya vinywaji na kutupwa hovyo barabarani.

“Wahusika wakuu wa hizi taka ni wafanyabiashara, lakini leo tunakwenda kufanya usafi na kuzibua mitaro wao wanafunga maduka na kukimbia, sasa nimeamuru kila mbele ya duka paachwe na uchafu wake,” ameng’aka Kaganda na kuongeza;

“Hivyo mkurugenzi nakuagiza, hakikisha hao watu hafungui maduka yao hadi wafanye usafi mbele ya maeneo yao lakini watoe faini ya kuchafua mazingira maana haiwezekani watukimbie badala ya kutusaidia.”

Akizungumzia hali hiyo, diwani wa viti maalumu, Faraja Emmanuel amesema watahakikisha agizo hilo la  Mkuu wa Wilaya linatekelezwa sambamba na kuongeza siku za kufanya usafi  katika maeneo yao.

“Kipindi hiki ambacho mvua bado inaendelea, itabidi mkuu hili suala la usafi liwe mara mbili kwa wiki ili kunusuru mitaro yetu isizibe na kusababisha maafa kwa wananchi wetu, lakini pia kuchukua tahadhari ya magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusababishwa na uchafu.

Related Posts