Morogoro. Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama amesema wanamshikilia dereva wa basi la Shabiby namba T341 EEU, Said Malugula mkazi wa Dar es salaam baada ya kusababisha ajali iliyotokea saa 12:20 asubuhi ya leo Mei 25,2024 eneo la Kihonda kwa Chambo.
Gari hilo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea mkoani Dodoma.Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Kamanda Mkama amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo, ambaye alikua anayapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.
“Tunamshikilia Sadick Said Malugula dereva wa basi la Shabiby T341 EEU ambaye amesababisha ajali eneo la Kihonda kwa Chambo baada ya kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, ambapo gari hilo liliacha njia na kupinduka.”
“Kwenye gari hilo kulikuwa na abiria 57, kutokana na ajali hiyo miongoni mwao kuna majeruhi 22 waliofikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa uangalizi,”amesema Mkama na kuongeza.
“Kati ya hao abiria watano wanafanyiwa vipimo huku wengine wametibiwa na kuruhusiwa.”
“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva maana eneo lile la Kihonda kwa Chambo kuna makatazo ya kuyapita magari mengine, lakini yeye akawa anafanya hivyo kwenye eneo lile likiwa na mstari wenye makatazo na mbele yake kukawa na bajaji inashuka, akalazimika kukwepa pembeni akakuta ukingo na gari ikapinduka,”amesema Kamanda Mkama.
Akizungumzia hali ya majeruhi Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Nafsa Malumba amesema wamepokea majeruhi 22 waliopata ajali na basi la Shahiby
“Majeruhi ambao hali zao sio nzuri wako watano, watatu wakiwa na mivunjiko mbalimbali na wawili wanasumbuliwa na mgongo, wengine wote wana majeraha madogomadogo na tumeshawapatia huduma ya kwanza, kuna watakaolazwa na tutakaowaruhusu” amesema Malumba
Akizungumza na Mwananchi Digital mmoja wa abiria aliyekuwa kwenye basi hilo, Aliko Emmanuel Masaga amesema ajali hiyo imesababishwa na bajaji iliyokatiza ghafla mbele ya basi hilo ambalo lilikuwa kwenye mwendo wa kasi kuyapita magari mengine.
“Tumeanza safari salama lakini tulivyotoka hotelini kuja maeneo haya ya Kihonda ilitokea dereva wetu akayapita malori lakini bahati mbaya zikatokea bajaji mbili mbele katika kuzikwepa akashindwa mwisho akaingia kwenye gema na basi kupinduka, tunamshukuru Mungu wengi tumepona hakuna kifo lakini wako ambao wameumia mikono, mgongo na miguu” amesema
Hamis Shaban ni majeruhi katika ajali hiyo ambaye amesema baada ya ajali hiyo amepata maumivu makali kwenye kiuno, ambapo hadi sasa hawezi kutembea
“Tulipofika Msamvu Stand kuna abiria walishuka na baada ya hapo tukaenda hotelini kujisaidia na kuanza safari kabla ya kuvuka kilima cha mwendokasi Kwa Chambo kuna malori yalikuwa yamepaki kushoto na kidogo dereva alikua kasi sio siri, ghafla akatokea mwenye bajaji kwenye kumkwepa ndio gari ikaanguka.”
“Majeraha niliyonayo mimi ni kiunoni kwa sababu baada ya gari kuanguka nilidondoka kutoka upande wangu wa kushoto nikarushwa kwenye kiti kingine nikajigonga kwenye kiuno hapo nikasikia maumivu makali nikajaribu kuinuka kuagalia vitu vyangu nikavipata, baada ya hapo nikajikuta hata kutoka kwenye basi siwezi tena kutokana na maumivu kuwa makali baadaye nilitoka kadri muda ulivyokwenda maumivu yakazidi mpaka nikashindwa kutembea na sasa nangojea vipimo nijue nimeumia kwa kiasi gani,”amesema.
Emmanuel John Lyimo shuhuda wa ajali hiyo amesema alichoshuhudia ni basi la Shabiby kuyapita magari mengine na kutaka kumgonga dereva bajaji
“Mimi ni dereva bodaboda na shughuli zangu zinafanyika hapahapa ilikua saa 12 :20 asubuhi nikaona basi la Shabiby likiyapita magari mengine na kutaka kumgonga dereva bajaji wakati anakwepa akatoka nje ya barabara akaanguka, lakini hakuna aliyefariki baada ya hapo tukaja kuokoa watu wakapelekwa hospitali” amesema Lyimo
“Tunawaomba madereva waongeze umakini kwenye kuendesha magari na wafuate sheria maana siku hizi ajali za barabarani zimekuwa zikisababishwa na madereva kuendesha vyombo vya moto kwa mbwembwe jambo ambalo ni hatari”
Majuto Mahimbali ni meneja wa Mabasi ya Shabiby kutokea Dodoma amesema baada ya ajali hiyo kutokea majeruhi wote watapewa huduma stahiki mpaka watakapomaliza safari.
“Kweli tumepata ajali basi letu limeanguka hapa Morogoro na kwa kuwa kuna majeruhi wamepatikana na walikuwa hawajamaliza safari zao tutahakikisha kwamba wanatibiwa na kumaliza safari zao kama ilivyokuwa imepangwa na gharama zote zitalipwa na Shabiby” amesema.