MAAFANDE wa Tanzania Prisons imejihakikisha kusalia katika Ligi Kuu Bara baada ya leo kupata sare ya 2-2 ikiwa ugenini mbele ya Namungo na kutuliza presha za mashabiki ambao mwanzoni mwa msimu waliishi kwa mawazo kutokana na timu kufanya vibaya.
Matokeo hayo yameifanya Prisons kufikisha pointi 34 na kusalia nafasi ya tano nyuma ya KMC, hivyo kuwa miongoni mwa timu zenye uhakika wa kushiriki ligi ijayo, kwani alama ilizonazo zimeziweka salama.
Mabao yaliwekwa kimiani na Khamis Zabona dakika ya 33 na Benedicto 61 yaliiweka Prisons katika nafasi nzuri ya kurejea Nne Boram, lakini wenyeji walipindua meza kwa kuchomoa moja baada ya jingine kupitia kwa Mrundi Derick Mukombozi aliyefunga dakika ya 58 na 84.
Prisons itajilaumu kwa kushinda kutoka na ushindi mjini Lindi, kwani iliongoza kwa muda mrefu na kupanda nafasi ya nne ikiing’oa KMC, kabla ya bao la Mukombozi kuitibulia na kuifanya iambulie sare hiyo na pointi moja.
Katika mechi nyingine iliyopigwa mjini Singida, wenyeji Ihefu ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Dodoma Jiji katika pambano la Dabi ya Kanda ya Kati.
Mabao ya washindi yalifungwa na Yassin Mgaza dakika ya saba na Mghana Christian Zigah aliyetupia dakika moja kabnla ya filimbi ya mwisho na kuifanya Dodoma kufikisha pointi 33 ikilingana na Namungo, Singida na Ihefu.