Mvua kubwa zilizonyesha nchini Kenya, Tanzania na mataifa jirani zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 500, na kuwalaazimu mamia ya maelfu kuyahama makazi yao huku mafuriko yakisomba nyumba na kuvunja barabara wakati wa msimu wa masika kuanzia mwezi Machi hadi Mei.
Kanda hiyo pia ilikumbwa na mafuriko mwishoni mwa mwaka jana, huku watafiti wakisema kuwa Dipole ya Bahari ya Hindi (IOD), ambayo ni mfumo wa hali ya hewa unaofafanuliwa na tofauti ya joto la uso wa bahari kati ya maeneo ya magharibi na mashariki mwa bahari — ilichangia mvua kubwa.
Mvua za mwaka huu ziliaminika kuwa zilichochewa zaidi na El Nino — hali ya hewa inayohusishwa na ongezeko la joto ambalo husababisha ukame katika baadhi ya maeneo ya dunia na mvua kubwa kwingineko.
Lakini utafiti uliochapishwa na shirika la World Weather Attribution (WWA) siku ya Ijumaa uligundua kuwa “watafiti hawakupata ushahidi wowote kwamba El Nino au Dipole ya Bahari ya Hindi vilikuwa na ushawishi wowote” juu ya mvua kubwa za mwaka huu.
Mtandao huo wa wanasayansi umebuni mbinu zilizopitiwa na wataalamu wenzao kwa ajili ya kubainisha kwa haraka jukumu linalowezekana la ongezeko la joto duniani katika matukio mahususi ya hali ya hewa kali.
Soma pia: Kenya: KHRC yawashtaki mawaziri kwa uzembe na kushindwa kuwalinda waathirika wa mafuriko
Wanasayansi walichunguza data za hali ya hewa na mifano ya tabianchi ili kulinganisha jinsi mifumo ya mvua ilivyobadilika kati ya sasa na enzi ya kabla ya viwanda, wakitafuta kupima athari za mabadiliko ya tabianchi kwa monsuni.
Sababu mchanganyiko
“Mvua iliyokithiri iliyosababisha mafuriko makubwa nchini Kenya, Tanzania na maeneo mengine ya Afrika Mashariki inazidi kuwa kubwa, huku mabadiliko ya tabianchi yakiwa moja ya vichochezi,” watafiti walisema.
“Makadirio bora zaidi ni kwamba mabadiliko ya htabianchi yalifanya tukio hilo kuwa mara mbili zaidi na asilimia tano kuwa kali zaidi,” walisema, na kuongeza tahadhari kwamba matokeo hayo pia yalipaswa kuzingatia “mashaka makubwa ya kihesabu”.
Utafiti huo ulihusu “kiwango cha juu cha mvua kwa siku 30” katika msimu wa masika wa mwaka huu, huku watafiti wakieleza kuwa “mvua kubwa itaendelea kuongezeka katika eneo hilo kutokana na ongezeko la joto.”
Utafiti huo umezitaka serikali katika eneo hilo kuboresha miundombinu na kulinda mifumo ya ikolojia ili kuokoa maisha na kuwasaidia wananchi kukabiliana na hatari kubwa ya majanga ya hali ya hewa, hasa katika maeneo ya mijini yenye watu wengi.
Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika ni miongoni mwa maeneo yaliyo hatarini zaidi na mabadiliko ya tabianchi — ingawa mchango wa bara la Afrika katika utoaji wa hewa ukaa duniani ni sehemu ndogo tu ya utoaji jumla wa gesi hiyo duniani.
Soma pia: Kenya, Tanzania zakabiliwa na kimbunga Hidaya
Zaidi ya watu 300 walikufa kutokana na mvua na mafuriko nchini Ethiopia, Kenya na Somalia mwishoni mwa mwaka jana, wakati eneo hilo lilipokuwa likijaribu kujikwamua kutokana na ukame mbaya zaidi katika miongo minne iliyoacha mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa.
Utafiti wa WWA kuhusu mafuriko ya mwaka jana katika kanda ya Afrika Mashariki ulitoa wito wa kukomeshwa kwa haraka kwa nishati ya mafuta na kupunguza utoaji wa hewa chafu duniani kote.