Fei Toto awahenyesha mashabiki wa Yanga kwa Mkapa 

WAKATI Yanga ikiwa uwanjani ikipambana na Tabora United, mashabiki wa timu hiyo walikuwa kwenye presha kubwa iliyotokana na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Presha ya mashabiki wa Yanga ilitokana na kufuatilia kwao mchezo wa Azam FC na Kagera Sugar uliokuwa unapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex,  ambao Fei Toto alikuwa tayari amefunga mabao mawili.

Wakati Fei Toto akiwa na mabao mawili, nyota wa Yanga, Stephane Aziz KI alikuwa hajafunga bao, hivyo kimahesabu kiungo huyo wa Azam alikuwa ameshafikisha 18 na kumzidi bao moja staa huyo wa Yanga aliyekuwa na 17.

Ghafla katika dakika ya pili ya nyongeza, Azizi Ki aliwaondoa mashabiki wa timu hiyo katika simanzi baada ya kufunga bao la kichwa ambalo lilihitimisha ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United.

Bao hilo la Aziz Ki linakuwa la 18 akiendelea kukabana koo na Fei Toto kila mmoja akisaliwa na mechi moja kufunga msimu zitakazopigwa Jumanne ijayo.

Mechi hizo ambapo Yanga itakuwa nyumbani dhidi ya Prisons na Azam ikiwa ugenini dhidi ya Geita Gold ndizo zitaamua nani atamzidi mwenzie kati ya Fei toto na Azizi Ki zitakazochezwa Mei 28 kwenye kufunga pazia la Ligi Kuu Bara.

Aziz Ki kabla ya mechi dhidi ya Tabora United na Feisal tayari alishafikia rekodi ya msimu uliopita ndani ya Yanga na katika Ligi Kuu ya Fiston Mayele aliyekuwa Yanga na Saido Ntibazonkiza wa Simba waliofunga mabao 17 kila mmoja na kwa kufikisha 18 yeye na Fei Toto wameivunja kabla ya msimu haujafungwa.

Mabao hayo kwa Fei yamemfanya aifikie rekodi ya Mrisho Ngassa alipokuwa na kikosi hicho msimu wa 2010-2011 alipofunga 18 akiweka rekodi kabla ya John Bocco aliyepo Simba kuivunja msimu uliofuata 2011-2012 akitupia 19, idadi ambayo kiungo huyo aliyesajiliwa kutoka Yanga kasaliwa na bao moja kuifikia.

Related Posts