Frateri aliyejinyonga azikwa bila sala, mama ashindwa kuhudhuria

Moshi. Wakati mamia wakijitokeza kumzika Frateri Rogassian Massawe anayedaiwa kujinyonga, mama yake mzazi, Levina Hugo ameshindwa kuhudhuria maziko hayo.

Frateri huyo ambaye amezikwa leo Jumamosi Mei 25, 2024 nyumbani kwao katika Kijiji cha Umbwe Onana wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, anadaiwa kujinyonga Mei 20, 2024 kwa kutumia mshipi akiwa kwenye nyumba yao ya malezi ya Magambo iliyoko wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Inadaiwa, kabla ya kujinyonga Frateri Massawe aliandika ujumbe wa maandishi kwenye karatasi na kuuacha mezani ukisema; “Mama usilie, nimeshindwa kufikia malengo, ninajua nimewakwaza wengi.” 

Hata hivyo, Frateri huyo wa Shirika la Roho Mtakatifu la Kanisa Katoliki, amezikwa bila kufuata taratibu za Kikatoliki, ambazo haziruhusu mtu aliyejinyonga kusomewa ibada ya maziko.

Akizungumza katika maziko hayo, Paroko wa Parokia ya Utukufu wa Msalaba, Jimbo Katoliki la Moshi, Anicet Alipenda amewaomba waombolezaji kuiombea familia ya frateri huyo kwa kuwa mama yake mzazi Levina bado amelazwa hospitalini kutokana na mshtuko alioupata baada ya kupokea taarifa za kifo hicho.

Amesimulia namna alivyokuwa akimfahamu Frateri Massawe, kuwa alikuwa akiutamani sana u padri tangu akiwa mdogo.

“Labda niwaambie kitu ambacho mnaweza kusema ni kichekesho kidogo, licha ya kuwa tupo kwenye maombolezo, kuna kipindi alipokuwa akisoma filosofia, alikuja parokiani kwa likizo, siku moja akaingia sakristia (chumba cha kuvalia mavazi ya misa) akamwambia sista aliyekuwepo, naomba kanzu nivae.”

“Naye sista akampa kanzu iliyokuwepo, sasa mimi nikamkuta ameivaa, nikamwambia Marunda (Rogassian) umetoa wapi hii kanzu, akaniambia padri nimeivaa, nikamwambia hapana vua, nikamwambia ukiivaa hii kabla ya wakati uliokubalika wakigundua watakwambia wewe acha,” amesimulia padri huyo.

Hivyo, anasema alipomwambia vile, aliondoka akiwa anahuzunika. “Nikamwambia Marunda mpaka nielezwe rasmi kwamba sasa shirika limekuruhusu, ndiyo utaanza kuvaa kanzu, lakini bado alionekana kusononeka.”

Anasema Massawe alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuwa padri, lakini mapenzi ya Mungu yaachwe yatimizwe.

Anasema ni wazi kuwa kifo hicho kimeacha huzuni kwa familia, parokia, kanisa na jamii kwa ujumla, hivyo akawataka watu wote kutomhukumu frateri huyo kwa kilichotokea bali wamwachie Mungu ndiye ajuaye kila jambo.

“Ni kifo ambacho kimetia huzuni, familia imehuzunika, parokia imehuzunika na kanisa limehuzunika na kila mtu mwenye nia njema na mapenzi mema amehuzunika, lakini kwa sababu tuna imani, kila atakayeishi vizuri na kufa mikononi mwa Mungu atamwendea Mungu, atamuona muumba wake,” amesema padri huyo.

Akizungumza katika maziko hayo, kaka wa Massawe ambaye pia ni padri, Andrea Hugo amesema mdogo wake alikuwa anautamani sana upadri na Juni mwaka huu angetoka kwenye hatua aliyokuwa kwenda hatua nyingine ya kuweka nadhiri za awali.

Amesema tayari ilikuwa imeanza maandalizi ya  kuungana na mpendwa wao katika kutimiza lengo lake hilo.

“Mimi binafsi nilikuwa na dukuduku, nikisema nichukue likizo ya wiki mbili nije kuungana nao katika ule muunganiko wa nadhiri, lakini ndiyo hivyo,” amesema Padri Hugo.

Padri huyo aliwashukuru wale wote walioungana na familia yao huku akisema, “kwetu sisi upendo huu mkubwa mliotuonyesha hatuna budi kuwashukuru nyote na tunaomba mzidi kuiombea hii familia.”

Amesema mama yao ameshindwa kumzika mwanawe kwa sababu leo asubuhi alipelekwa hospitali na madaktari wakasema hawezi kurudi nyumbani, wanamlaza kutokana na hali yake kutokuwa nzuri.

“Presha imepanda na sukari nayo ipo juu sana, tumwombee na mtuombee kama familia,” amesema Padri Hugo.

Mmoja wa walimu aliyemfundisha mwanafunzi huyo kidato cha kwanza hadi cha nne katika Seminari ya Uru, aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema Massawe alikuwa  mwanafunzi mtulivu na alikuwa akifanya vema katika masomo yake mara zote.

“Darasani alikuwa mzuri sana, alikuwa mpole, kwa miaka ambayo amekaa pale shuleni sikuwahi kuona anapewa adhabu yoyote na hata alipoondoka hapa seminari, baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2016 tulikuwa hatutamani aondoke aende kwingine, tulitaka akae kule kwetu seminarini,” amesema mwalimu huyo.

Related Posts