WACHIMBA Dhahabu wa Geita, Geita Gold, wameendelea kujiweka pabaya katika Ligi Kuu Bara baada ya leo kufumuliwa mabao 2-1 na Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na sasa watalazimika kushinda mechi ya Jumanne mbele ya Azam iwapo hawataki kushuka daraja moja kwa moja.
Geita ipo nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 25 na kama itashinda itafikisha 31 na kusikilizia matokeo ya timu hiyo kuona itacheza play-off au itaungana na Mtibwa Sugar kwenda Ligi ya Championship baada ya mabingwa hao wa zamani kushushwa rasmi leo na Mashujaa.
Katika mechi hiyo, Singida inayopambana nayo kujiokoa na janga la kushuka daraja au kucheza play-off ilianza mapema kupata mabao kupitia kwa Nicholas Gyan aliyefunga dakika ya saba ya mchezo kabla ya Amos Kadikilo kuongeza jingine akimalizia pasi ya Deus Kaseke.
Geita ilipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 54 na Erick Kyaruzi akimalizia pasi ya Anthony Mlingo.
Ushindi huo umeifanya Singida kufikisha pointi 33 ikishika nafasi ya saba na sasa inajiandaa kuikaribisha Kagera Sugar ambayo leo imefumuliwa mabao 4-1 na Azam jijini Dar es Salaam.