ZIKIWA zimesalia saa tatu tu ili mechi muhimu kati ya Yanga na Tabora United ichezwe, mashabiki nao hawapo nyuma.
Yanga leo inaikaribisha Tabora United katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa ni mechi ya 29 katika ligi msimu huu, ikiwa imebakiza mchezo mmoja mkononi katika mechi itakayoanza saa 10:00 jioni.
Wanajangwani hao watakabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2023/2024, wakifikisha rekodi ya kuchukua ushindi huo mara tatu mfululizo.
Nje ya uwanja zimetawala rangi mbili tu njano na kijani, huku biashara zikiwa zinaendelea taratibu na mashabiki wengine wakionekana barabarani na magari wakikaribia eneo hilo.
Ni wazi kuwa mwitikio wa mashabiki umeonekana kuwa mkubwa, lakini wengi wao wakionekana kujiamini kwani wanajua kuwa wanakwenda kupata kile walichokuwa wanakitamani tangu msimu ulipoanza.
Hali ya usalama iko vizuri, lakini utulivu pia ni mkubwa, huku wanaoingia ndani wakiwa sio wengi na kupelekea kutokuwa na foleni kubwa.
Ikumbukwe msimu uliopita Yanga ilipata ubingwa huo wakiwa chini ya kocha Nassridine Nabi ambaye kwa sasa anaifundisha FAR Rabat ya Morocco.
Lakini Tabora United inaingia na kumbukumbu mbaya katika mchezo wa leo kwani ilipokea kipigo cha mabao 1-0 ikiwa nyumbani, huku ilitakiwa kushinda mechi hiyo dhidi ya Bingwa ili ijiondoe kwenye eneo la kushuka daraja.