Luvanga arejeshwa Twiga Stars | Mwanaspoti

BAADA ya kukaushiwa kwa muda mrefu, hatimaye mshambuliaji nyota wa timu ya soka ya wanawake ya  Al Nassr ya Saudi Arabia, Clara Luvanga amejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 21 wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars kinachotarajia kushiriki mashindano maalumu.

Clara aliyetwaa taji la Ligi Kuu ya Saudia akiwa na Al Nassr yenye timu ya wanaume pia anayoichezea nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo hajaitwa timu ya taifa tangu alipocheza mara ya mwisho kikosi cha U17, Serengeti Girls katika mechi za mchujo za Fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyikia India.

Licha ya kuivusha timu hiyo kwenda India kwa mabao 10 aliyofunga yakiwamo dhidi ya Cameroon iliyoleta zengwe, nyota huyo wa zamani wa Yanga Princess na Dux Logrono ya Hispania hakuwepo katika fainali hizo za India ambapo Tanzania iliishia robo fainali ikifungwa mabao 3-0 na Colombia.

Clara anaungana na Maimuna Khamis ambaye naye alikuwa hajaitwa kwa muda mrefu katika kikosi cha timu ya taifa sambamba na nyota wengine 19 ili kuunda kikosi hicho cha wachezaji 21 kilichoingia kambini jana tayari kwa maandalizi ya mchezo huo maalumu utakaochezwa mwisho wa mwezi huu.

Wengine walioitwa ni Najat Abbas (JKT Queens), Asha Mwisho (Amani Queens), Lidya Maximilian (JKT Queens), Christer Bahera (JKT Queens), Janeth Singano (Juarez, Mexico), Enekia Kasonga (Eastern Flames), Janeth Pangamwene (JKT Queens), Vaileth Nicholaus (JKT Queens) na Joyce Lema (JKT Queens).

Pia wamo Suzan Adam (Tuthankhamun), Esther Maseke (Bunda Queens), Diana Lucas (Ame S.F.K, Uturuki), Oppa Clement (Besiktas), Jamila Rajab (JKT Queens), Winfrida Gerald (JKT Queens), Aisha Masaka (BK Hacken), Stumai Abdallah (JKT Queens), Aisha Juma (Simba Queens), Aliya Fikiri (JKT Queens) na Asha Ramadhan (Yanga).

Clara aliyezaliwa Februari 25, 2005 amewahi kuwa Mchezaji Bora wa Kike wa Tanzania msimu wa 2022/23, Mchezaji Bora Chipukizi wa Kike 2021-2022 na kuteuliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Chipukizi wa Afrika kupitia CAF 2022 na safari hii akiwa na Al Nassri ameifungia mabao 11 na kusaidia kuipa taji la pili la Ligi.

Related Posts