Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imewaruhusu Shose Sinare, Harry Kitilya na Sioi Solomon kupinga hukumu iliyowatia hatiani katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili.
Mahakama imewaruhusu kufungua shauri la maombi, kuiomba Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi itengue hukumu yake iliyotokana na kukiri kwao makosa kutokana na makubalino (plea bargaining), baina yao na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Agness Mgeyekwa na Amour Khamis, Alhamisi Mei 23, 2024 kutokana na rufaa waliyokata wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Walikuwa wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kutupilia mbali shauri lao la maombi ya kuongezewa muda wa kufungua shauri la kuomba kutengua hukumu hiyo iliyowatia hatiani, baada ya kuchelewa kufungua shauri hilo.
Mahakama ya Rufani katika uamuzi imesema baada ya kupitia uamuzi uliokuwa unapingwa, imebaini Mahakama Kuu imetambua kuwa kuchelewa kupata nakala za nyaraka husika ni moja ya sababu ambazo mahakama inazizingatia.
Pia imesema Mahakama Kuu ilitambua kuwa uzembe huo ulisababishwa na Mahakama yenyewe, kushindwa kuwapatia nakala za nyaraka hizo kwa wakati.
Hivyo, Mahakama ya Rufani imesema imeridhika kuwa kina Kitilya walitoa sababu ya kuridhisha ya kuchelewa kwao.
Walieleza walichelewa kufungua shauri hilo kutokana na kuchelewa kupata nakala za nyaraka muhimu, ikiwemo hukumu inayopingwa.
Mahakama ya Rufani imesisitiza kuwa kwa kutazama tu uamuzi unaopingwa, warufani wameonyesha sababu sahihi ya kuongezewa muda na kwamba ikiwa ndivyo, inaona sababu ya warufani kuongezewa muda ilikuwa na mashiko na inatosha kuamua rufaa hiyo.
“Kwa hiyo tunatumia mamlaka yetu chini ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri la maombi ya uhujumu uchumi namba 2 la mwaka 2022 na tunakubali rufaa ya warufani,” imesema Mahakama ya Rufani na kuamuru:
“Warufani wanapewa siku 30 kufungua shauri la maombi linalokusudiwa (kuomba kutengua hukumu iliyowatia hatiani)”.
Katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi namba 4 ya mwaka 2019, Kitilya, Shose, Sioi, na wengine wawili, waliokuwa maofisa wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda na Alfred Misana, walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 58.
Mashtaka hayo yalikuwa ni ya kuongoza uhalifu wa kupangwa, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kumdanganya mwajiri kwa kutumia nyaraka, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu (Dola za Marekani 6 milioni), utakatishaji fedha hizo na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Walikuwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi, wakati wa mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingireza.
Wakati huo, Kitilya alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors Limited (EGMA) iliyokuwa inajishughulisha na ushauri wa uwekezaji, huduma za uwezeshaji na upatikanaji wa fedha, ambayo ndiyo ilikuwa inadaiwa kutumika kujipatia fedha hizo.
Shose alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Uwekezaji wa Stanbic Bank Tanzania Ltd na Sioi alikuwa Mkuu Idara ya Sheria na Katibu wa benki hiyo.
Shallanda na Missana walikuwa watumishi wa Wizara ya Fedha, waliokuwa wanahusika na masuala ya mikopo ya Serikali.
Shallanda alikuwa Kamishna wa Uchambuzi wa Sera na Misana alikuwa Kamishna Msaidizi wa Usimamizi wa Madeni.
Agosti 25, 2020 walitiwa hatiani baada ya kukiri makosa kutokana na makubaliano baina yao na DPP.
Walihukumiwa adhabu ya kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja na fidia ya Sh1.5 bilioni kama walivyokubaliana baada ya majadiliano baina yao na DPP.
Machi 30, 2022, takribani miaka miwili baada ya hukumu, Kitilya, Shose na Sioi walifungua shauri la maombi ya kuongezewa muda ili wafungue shauri la maombi ya kutengeua hukumu hiyo; yaani hatia, adhabu na amri za Mahakama.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, walidai walichelewa kufungua shauri la kutengua hukumu kwa kuwa walikuwa wanasubiri kupatiwa nakala za mwenendo wa kesi walizoomba tangu Oktoba 5, 2020.
Mahakama Kuu katika uamuzi ilioutoa Agosti 19, 2022 ilikubaliana na hoja za Serikali na ikayatupilia mbali maombi ya kuongezewa muda ikieleza pamoja na mambo mengine, kwamba watoa maombi hawakutoa sababu za kuishawishi Mahakama kuwaongezea muda.
Mahakama katika uamuzi huo uliotolewa na Jaji Immaculata Banzi, ilikubaliana na hoja za Serikali kupiti kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa kuwa, namna majadiliano (na DPP) yalivyofanyika si sehemu ya mwenendo wa Mahakama, isipokuwa makubaliano yaliyowasilishwa mahakamani.
Alisema kwa kuwa tayari walikuwa na nakala ya makubaliano hayo waliyoyasaini, hapakuwa na haja ya kusubiri kupata mwenendo wote wa kesi, ukiwemo ushahidi wa mashahidi waliokuwa wameushatoa, katika kuthibitisha hawakukubali kwa hiari au kuwakilishwa kwao katika majadiliano hayo.
Kutokana na uamuzi huo walikata rufaa wakiwasilisha sababu sita kuonyesha Mahakama ilikosea kutupilia mbali maombi yao.
Siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, wakili wao Zaharani Sinare aliomba na akaruhusiwa na Mahakama kuondoa sababu hizo kisha akawasilisha moja, kwamba Mahakama Kuu ilikosea katika uamuzi kwa kutumia kifungu cha 43 (a) cha Sheria ya Ukomo.
Alidai kifungu hicho hakitumiki katika kuamua mashauri ya jinai, huku akiirejesha Mahakama katika uamuzi wake kwenye kesi nyingine kuhusu hoja hiyo, kuwa kifungu hicho hakitumiki katika mashauri ya jinai.
Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Mkuu, Zakaria Ndaskoi, ingawa alikiri kuwa kifungu hicho hakitumiki katika mashauri ya jinai, alidai uamuzi wa Mahakama Kuu haukuwa na makosa.
Aliunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu kuwa warufani walishindwa kutoa sababu za kuridhisha kuishawishi mahakama kuwaongezea muda kufungua shauri hilo la kupinga hukumu iliyowatia hatiani.
Mahakama ya Rufani katika uamuzi imesisitiza masharti ya Sheria ya Ukomo hayatumiki katika kuamua mashauri ya jinai, na ikahitimisha kuwa kwa kusoma uamuzi uliokuwa unapingwa, warufani walitoa sababu yenye mashiko ya kustahili kuongezewa muda.