Karatu. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba kusimamia kazi ya kutoa maji na kujenga mitaro ifanyike usiku na mchana katika Mtaa wa Mangafi ili nyumba 502 zilizofunikwa zaidi ya mwezi mmoja zirejee kwenye hali yake ya kawaida.
Katika mtaa huo mpaka sasa kaya 889 zenye wananchi zaidi ya 2,800 wameathirika na mafuriko hayo na miundombinu mbalimbali ikiwemo visima viwili vya maji vikiwa vimefunikwa na kusababisha wananchi 7,638 kukosa huduma ya maji.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Mei 24, 2024 katika ziara ya Makonda wilayani humo ambaye licha ya kutembelea miradi ya maendeleo, amekagua eneo hilo ambalo limefunikwa na maji tangu Aprili 8, mwaka huu.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa eneo, amemtaka Kolimba kusimamia kazi hiyo ifanyike usiku na mchana ili wananchi hao waweze kurejea katika makazi yao.
Katika hatua nyingine, Makonda amesema nyumba zilizoathiriwa zipo jirani na bwawa la Karatu, ni vema wananchi wakatafuta mbadala mwingine wa makazi badala ya kung’ang’ania kuishi kwenye eneo hilo alilosema ni hatarishi kwao.
“Nimepita kila mahali, kwa kweli tunawapa pole wananchi, nitatafuta namna ya kuwasaidia viongozi wa wilaya ili kuwapa ninyi faraja, tuna magodoro, vyakula, tutaleta kwa uongozi wa wilaya ili wawaletee,” amesema makonda.
Awali, akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Diwani wa Karatu ulipo mtaa huo, Joseph Lolo amesema kutokana na mvua kubwa zilizonyesha, eneo hilo lilikumbwa na mafuriko hayo tangu Aprili 8, mwaka huu na kuathiri kaya zaidi ya 889 zenye wananchi zaidi ya 2,800.
Ametaja athari nyingine zilizotokana na mafuriko hayo ni nyumba 31 kudondoka,visima viwili vya maji kufunikwa hivyo kusababisha wananchi 7,638 kukosa huduma ya maji pamoja na transfoma tatu kuharibiwa na kusababisha wananchi kukosa umeme.
“Kwa kweli kama hali inavyoonekana hapa nyumba 502 hadi sasa zimefunikwa na maji na suluhu ya kudumu kimsingi ni kuwekwa kwa matoleo ya maji kwa sababu bwawa letu halikuwa na sehemu ya kupumulia maji,hivyo maji yalivyojaa bwawani yamekuja kufunika na kuharibu makazi ya watu,” amesema.
Mkuu wa wilaya hiyo, alisema wameshafanya vikao vya tathmini na wameshapeleka mitambo katika eneo hilo na changamoto ilikuwa kaya tatu ila kwa maelekezo ya mkuu huyo mkoa, mitambo itaanza kazi mara moja.
Mmoja wa wananchi hao ambaye nyumba yake imefunikwa, Paulo Filbert, ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kutoa maji hayo ili waweze kurejea katika makazi yao.
Amesema kwa sasa wanaishi kwa ndugu na jamaa huku mali zao nyingi zikiwa zimefunikwa ndani ya maji hayo ikiwemo nyumba, magari na samani nyingine.