Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki amesema miongoni mwa viashiria vya kuvunjika kwa amani barani Afrika ni nchi wanachama kutozingatia matakwa ya kidemokrasia ya kuwa na chaguzi huru na za haki.
Amesema licha ya kuwa na Baraza la Amani na Usalama (PSC), AU haina uwezo wa kuziwekea vikwazo nchi wanachama zinazokiuka katiba na itifaki za baraza hilo.
Faki ameyasema hayo leo Mei 25, 2024 alipokuwa akihutubia katika mkutano wa maadhimisho ya miaka 20 ya PSC jijini Dar es Salaam, akisema kuna haja ya kufanya tathmini kuhusu katiba na itifaki iliyoanzisha baraza hilo kuhusu uchaguzi na demokrasia kwa Afrika.
“Kumekuwa na changamoto ya mabadiliko yasiyozingatia katiba na haya hayavumiliki kabisa.”
“Mfano, ibara ya 19 ya mkataba kuhusu uchaguzi na utawala kwa wazi kabisa inatangaza, kila mwanachama anatakiwa kutoa ratiba ya uchaguzi na kuruhusu waangalizi. Je, ni nchi ngapi zimekuwa na ratiba na kualika waangalizi?” amehoji.
“Tuseme nini kwa mabadiliko yanayotokea Afrika ambayo majeshi yanagombea kwenye uchaguzi? Tunajua leo, wote watagombea na watadai kuwa wameshinda?” amehoji.
Amesema licha ya itifaki za baraza hilo kuweka miongozo ya kuheshimu mabadilishano ya uongozi kwa amani, baadhi ya nchi haziheshimu.
“Naomba tukubali kwamba PSC, inashindwa kuweka vikwazo wakati hayo yanapotokea hasa kuzuia mabadiliko yasiyo ya kikatiba katika nchi mbalimbali,” amesema.
Hata hivyo, amesema wataendelea kuchukua maamuzi magumu ili kukabiliana na ukiukwaji wa miongozo ya amani katika chaguzi.
Akizungumzia mafanikio ya PSC kwa miaka 20, Faki amesema baraza hilo limeweka kanuni za amani na usalama katika bara hili ambayo suluhisho la kukabiliana na migogoro na kukuza maridhiano.
“Kumekuwa na jitihada za kutatua migogoro kama DRC, Comoro, Ivory Coast, Ethiopia, Libya, Somalia na Sudan Kusini. Kumekuwa na ushirikiano kati ya PAC na Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa na katika kulinda amani na usalama,” amesema.