SHAMRASHAMRA za Pati la Likipigwa zikiendelea kwa sasa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkaja, jijini Dar es Salaam, nje kidogo ya uwanja huo utakaotumika kwa mechia ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Tabiora United, biashara zimeanza kuchangamka maeneo tofauti na kuwa neema kwa wafanyabiashara.
Yanga inatarajiwa kukabidhiwa taji la 30 la Ligi Kuu Bara tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965 ikiwa ni mara baada ya kumalizana na Tabora na shangwe la pati hilo la klibingwa limeanza tangu saa 4 asubuhi.
Kwa sasa ikiwa ni mchana katika maeneo tofauti nje ya uwanja huo watu wamekuwa wakiingia sehemu mbalimbali kupata vyakula na vinywaji.
Kuna wafanyabiashara wenye vibanda vya kuuza vyakula na wale walioweka meza barabarani ambavyo kumekuwa na msururu wa watu kutaka huduma hizo ikiwamo maji, soda na jezi za klabu mbalimbali za soka pia zikiendelea kuwaneemsha wachuuzi wake.
Akizungumza na Mwanaspoti mmoja wa wauza vyakula, Hadija Ahmed alisema hadi saa saba mchana tayari ameuza sufuria tatu ambapo kwa kawaida hutumia siku mbili hadi tatu kuuza.
“Hapa nimemaliza lakini muda bado kwa hiyo ninapo pika nimewatuma waongeze sufuria tatu kwa sababu ndio kwanza shughuli imeanza bado hadi usiku,” alisema Hadija.
Nje na wauza vyakula wapo pia wanaofanya biashara za usafiri (waendesha pikipiki) ambao wanapiga safari za kuwapeleka watu sehemu moja kwenda kukata tiketi.
John maarufu Chama ni mmoja wa waendesha bodaboda ambaye anasema amebeba zaidi ya abiria 10 ambao anawapeleka sehemu ya kukatia tiketi za mchezo.
“Mimi nimetega eneo la watu wanapopita sana, kuna mashabiki hawajui sehemu za kukata tiketi ninachofanya natumia fursa hiyo kuwapeleka wananipa Sh elfu moja ya kuwapeleka na bodaboda maana sio mbali,” alisema Chama.
Mbali na mechi hiyo ya Kwa Mkapa, lakini leo zinapigwa pia michezo mingine saba ya Ligi Kuu ambapo Simba itakuwa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha kumalizana na KMC, wakati Azam na Kagera Sugar zenyewe zitavaana Uwanja wa Azam Complex.
Mechi nyingine za leo jioni ni zile za Singida FG dhidi ya Geita Gold utakaopigwa Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza, Wagosi wa Kaya, Coastal Union itakayoikaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga na Ihefu itaialika Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida.
Mashujaa itakuwa wenyeji wa vibonde, Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjinui Kigoma na Namungo itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Wakati Yanga tayari ikiwa imeshatangaza ubingwa ikiwa na michezo mitatu mkononi, Azam na Simba zenyewe zitakuwa zikisikiliziana katika kuwania nafasi ya pili na kukata tiketi ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Coastal Union na KMC zenyewe zina vita yao ya kutaka kumaliza nafasi ya nne na kupata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika ikiungana na Bingwa wa michuano hiyo ambapo Azam na Yanga zimetinga fainali na zinatarajiwa kuvaana wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Bingwa pamoja na mshindi wa pili wa Ligi Kuu ndio wanayoiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati bingwa wa Kombe la Shirikisho na mshindi wa tatu hucheza Kombe la Shirikisho Afrika, lakini iwapo bingwa wa Ligi Kuu akiwa pia ni bingwa wa FA hutoa nafasi kwa mshindi wa nne wa Ligi Kuu kuungana na mshindi wa tatu kucheza Shirikisho Afrika kama ilivyojitokeza misimu kadhaa sasa.
KMC, Namungo, Geita Gold, Biashatra United na Singida FG zilikata tiketi hiyo kutokana na Simba na Yanga kubeba mataji yote mawili kwa msimu mmoja na kuzifanya timu hizo zishiriki michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.