Uhusiano kati ya CCM, CPC fursa ya kutangaza utalii

Unguja. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema kuimarika kwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya chama hicho na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ni fursa kwa Zanzibar kutangaza sekta ya utalii kimataifa.

Amesema hayo katika mazungumzo na ujumbe maalumu wa CPC yaliyofanyika ofisini kwake Kisiwandui, Unguja Mei 24, 2024.

Amesema Zanzibar ni nchi ya visiwa ambayo uchumi wake unategemea zaidi sekta ya utalii, hivyo ni muhimu kwa China kuleta raia wake Zanzibar kufanya utalii na uwekezaji.

Dk Dimwa amesema CCM inathamini na kutambua mchango wa CPC katika masuala ya maendeleo yanayotekelezwa na China kwa dhamira ya kuunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Amesema China imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa, kidiplomasia na kiteknolojia, hatua ambazo ni fursa ya kujifunza kwa lengo la kupata maarifa na ujuzi kutoka kwa Taifa hilo.

“Uhusiano wa kisiasa na kijamii kati ya CCM na CPC umeendelea kuimarika kutokana na misingi imara iliyoasisiwa na waasisi wa vyama vyetu ambao ni aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume na muasisi wa Chama cha Kikomunisti cha China, Mao Zedong,” amesema.

“Zanzibar ilipofanya mapinduzi mwaka 1964 nchi ya kwanza kutambua mapinduzi hayo ilikuwa China, hivyo inajivunia urafiki na ndugu zetu kwa kuwa ni busara; falsafa na mipango endelevu ya maendeleo iliyowekwa na viongozi hao ndiyo chachu ya ukuaji na ustawi wa vyama vyetu,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati Kuu ya CPC, Rao Huihua amesema chama hicho kimejipanga kuimarisha ushirikiano wa kisiasa baina yake na CCM.

Amesema CPC kupitia wataalamu wake wa vyuo vikuu wataendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa CCM kulingana na mahitaji yao ya kitaaluma na kisiasa.

Rao amesema Tanzania Bara na Zanzibar kwa jumla kuna vivutio vingi vya utalii vinavyotakiwa kupewa kipaumbele katika kuchangia ukuaji wa uchumi.

Related Posts