Ukosefu wa taarifa watajwa chanzo cha mikopo umiza

Geita. Kukosekana kwa taarifa sahihi za namna gani ya kupata teknolojia za kuzalisha bidhaa zenye ubora, yalipo masoko na namna ya kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha ni miongoni mwa changamoto zinazowakwamisha wajasiriamali wadogo kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogovidogo ( Sido) mkoa wa Geita, Nina Nchimbi wakati akizungumza na Mwananchi Digital kwenye maonyesho ya tano ya ‘Fahari ya Geita’ yaliyoandaliwa na kampuni ya African Creativity, yakilenga kuwaunganisha wafanyabiashara wadogo ili wajifunze kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Nchimbi amesema kutokana na wajasiriamali kukosa taarifa sahihi wengi huangukia kwenye mikopo umiza na kuishia  kufilisiwa mali zao, ilihali  wangeweza kukopa kwenye taasisi za fedha zinazotambuliwa na Serikali na kukopa kwa riba nafuu.

 “Maonyesho haya yamelenga kuwakutanisha wachimbaji, wakulima, wafagaji na wavuvi ambapo washiriki watapata mafunzo ya namna gani wanaweza kupata taarifa sahihi za mikopo, namna gani wazalishe bidhaa zenye ubora na wapi yalipo masoko.”

Nchimbi amesema kushiriki kwenye maonyesho hayo sio tu kutawasaidia kujifunza lakini kutawakutanisha na watu kutoka maeneo tofauti na kuwawezesha kupata fursa za kibiashara za ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia maonyesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Geita,  Hashim Komba amesema yatachochea uchumi wa mji wa Geita na kufungua fursa kwa wafanyabiashara mkoani humo kujifunza kutoka kwa wenzao wanaotoka ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Geita, Robert Gabriel amesema pamoja na Serikali kutunga sera nzuri bado mfanyabiashara mdogo hanufaiki kutokana na kukosa taarifa sahihi za namna gani ya kuendesha biashara, kupata soko na mtaji.

Amesema kupitia maonyesho hayo wajasiriamali watapata  mbinu ya namna gani ya kufanya biashara kwa tija lakini pia watawezaje  kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.

Eveline Bwire mkazi wa Chato amesema ujio wa wafanyabiashara kutoka nje ya mkoa huo unawasaidia kujifunza lakini pia kujua namna ya kukabiliana na changamoto za kibiashara.

Maonyesho hayo yatazinduliwa rasmi  kesho Mei 26, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella.

Related Posts