Dar es Salaam. Lishe duni ya vijana rika la balehe inatajwa kuwa chanzo cha matatizo ya afya ya uzazi miongoni mwa wanawake na wanaume.
Upungufu wa virutubisho muhimu kwa watoto na vijana unaelezwa kuathiri via vya uzazi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe, Wizara ya Afya, Neema Joshua anasema udumavu, uzito pungufu, ukondefu, uzito kupita kiasi na unene ni changamoto zinazowakabili watoto na vijana wenye umri wa miaka mitano hadi 19 nchini.
“Matokeo ya tathmini ya malaria na hali ya lishe kwa wanafunzi wenye umri wa miaka mitano hadi 19 ya mwaka 2019 yanaonyesha asilimia 25 ya wanafunzi wa umri wa miaka 10 hadi 19 walikuwa wamedumaa,” anasema.
“Tathmini ilibainisha asilimia 33.7 ya wanafunzi wenye umri wa miaka 5-19 walikuwa na tatizo la upungufu wa damu, asilimia 6.2 walikuwa wanene kupita kiasi na asilimia 11.2 walikuwa wakondefu,” anasema Neema.
Anaeleza utafiti ulibainisha asilimia 42 ya vijana wenye umri wa miaka 10-19 walikuwa na kiwango cha chini cha kushughulisha mwili au kutofanya mazoezi.
Makadirio kidunia yanaonyesha kuna vijana bilioni 1.2 wenye umri wa miaka 10-19 wanaongezeka kwa kasi kubwa, huku Tanzania ikikadiriwa kuwa robo ya watu wote ni vijana wa rika balehe.
Ulaji usiofaa wa vyakula ni tatizo kwa rika balehe miongoni mwa kaya na zaidi katika shule za kutwa na bweni za Serikali na binafsi.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini wanafunzi wanalishwa vyakula vya aina moja kwa muda mrefu na vinakosa sifa ya ubora.
Hata kwa baadhi ya wanaoishi majumbani wamekuwa hawakuzwi kwa kuzingatia lishe bora, huku vijana wanaojitegemea, walio vyuo vya kati na vyuo vikuu baadhi yao chakula si kipaumbele, bali mavazi, simu na starehe.
Katika shule nyingi, ugali na maharagwe ndiyo chakula kikuu, mara chache hupewa matunda, nyama na mbogamboga.
Shule kadhaa zilizofikiwa na Mwananchi katika mikoa ya Iringa na Dar es Salaam imebainika wanafunzi wanakula ugali na maharagwe kwa siku sita za wiki vyakula vyenye wanga na protini pekee, hawapati mboga za majani.
“Tunakunywa uji wa mahindi kila saa nne asubuhi, mchana tunakula ugali na maharagwe, vivyo hivyo jioni. Jumapili ndiyo tunakula ubwabwa na nyama mchana lakini jioni ni maharagwe na ugali,” anasema mwanafunzi wa shule ya sekondari ya bweni mkoani Iringa aliyejitambulisha kwa jina moja na Jasmine.
Jasmine aliyesoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule ya bweni na sasa akiwa kidato cha tano, anasema mboga za majani na matunda hula akiwa nyumbani wakati wa likizo.
Ripoti ya awali ya TDHS ya mwaka 2022 inaonyesha viwango vya udumavu katika mikoa ya Iringa ni asilimia 59.9, Njombe (50.4) na Rukwa (49.8).
Kaimu Mkurugenzi Sayansi ya Chakula na Lishe katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk Analice Kamala anasema kipindi muhimu kwa binadamu ni siku 1,000 za mwanzo mpaka miaka mitano, kama mzazi au mlezi alikosea mwanzo kipindi muhimu ni rika balehe miaka 10 mpaka 19.
Anasema muda huo ni muhimu mtoto kupata madini joto, madini chuma na asidi ya foliki kwa kuwa ni umri wa kutengenezwa via vya uzazi na kutanuka vizuri, hivyo lazima apate madini na chakula kingi cha kutosha.
“Ikitokea changamoto yoyote katika nafasi hizo mbili, haiwezi kurekebishika na wasiopata lishe bora tangu utotoni hawafundishiki, hata akifikia umri wa kuzaa mtoto wake anazaliwa mwenye udumavu,” anasema.
“Umri huu wanahitaji chakula kingi ndiyo maana wanakula sana, msichana mwili unajitengeneza na mvulana hali kadhalika wanahitaji chakula kingi, huu ni umri ambao wanakua kwa kasi,” anasema Dk Kamala.
Anasema nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kuna upungufu wa vitamini A, madini ya chuma, madini joto, asidi ya foliki, B12 kwa kinamama wenye umri wa kuzaa watoto, hivyo walianzisha mkakati maalumu, ikiwamo kuongeza virutubisho kwenye chakula.
Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Fredrick Mashili anasema lishe ina umuhimu mkubwa katika umri wa miaka 9 hadi 19 kwani homoni nyingi zinazalishwa na mafuta yanayopatikana katika vyakula muhimu vikiwamo vyenye zinki.
Anasema mafuta na protini ni muhimu katika kupata homoni zinazofanya kazi katika kutengeneza viungo vya uzazi na afya kwa jumla.
“Mfumo mzima wa mwili unaotengeneza afya ya uzazi na via vyake ni lishe, tunaita virutubisho sababu vinatoka kwenye chakula, lazima kiwe na ubora na wingi unaotakiwa ili kufanya kazi katika afya ya uzazi na via vyake kwa ujumla,” anasema.
Dk Mashili anasema msichana akikosa lishe bora katika umri wa miaka 9 hadi 19 anakuwa amekosa virutubisho muhimu, hivyo anaweza kuwa na shida ya upungufu wa damu.
“Kwa wanaume homoni nyingi ambazo zinatumika kuimarisha via vya uzazi zinatengenezwa na mafuta ambayo ni mazuri kama vile Omega 3,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Mashili, ubora wa mbegu za mwanamume zenye uwezo wa kutungisha mimba, unatokana na alitunzwa vipi siku 1,000 za mwanzo, chini ya umri wa miaka mitano lakini zaidi ni katika umri wa balehe kwa mvulana wa miaka 9 hadi 19.
Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe, Wizara ya Afya, Neema Joshua anasema licha ya Serikali kutekeleza afua ya uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula ikiwamo unga wa mahindi, unga wa ngano, chumvi na mafuta ya kula, imeelekeza vyakula vinavyotumika shuleni viongezwe virutubisho ili kukidhi mahitaji ya lishe ya vijana balehe.
Neema anasema Serikali kupitia Wizara za Elimu na Afya ilitoa mwongozo wa chakula na lishe shuleni, unaopaswa kutekelezwa na shule zote za Serikali na binafsi ili watoto wa shule, wakiwamo vijana balehe wapate chakula na huduma zingine za kuwafanya wawe na afya na lishe bora.
Katikati ya changamoto hiyo, Wizara za Elimu, Tamisemi na Wizara ya Afya zinatekeleza afua ya utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni.
Jamii inahimizwa kuhakikisha kila mwanafunzi anapata angalau mlo mmoja anapokuwa shuleni.
Hata hivyo, katika baadhi ya mikoa, Iringa ukiwamo wazazi hawajahamasika kuchangia chakula cha watoto shuleni.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kihesa, iliyopo Manispaa ya Iringa, Edson Mwasenga anasema:
“Nina wanafunzi 1,074 ukihamasisha sana unapata wanafunzi wasiozidi 300, japo kwenye vikao tunakubaliana vizuri. Baadhi ya wazazi wanachangia lakini muda unavyokwenda idadi inapungua.”
Mwasenga anasema shuleni wanalima mbogamboga, na wanafuga kuku kwa ajili ya kuchangia mlo wa watoto. Pia kuna bwawa kwa ajili ya ufugaji wa samaki.
Ofisa Lishe Mkoa wa Iringa, Anna Nomba anasema walianzisha klabu shuleni ili kutoa elimu ya lishe, ulaji unaofaa, upungufu wa damu na mafunzo kwa vitendo. Anasema wameshazifikia shule 763 kati ya 767.
Anasema wapo mbioni kuwafikia wanafunzi wa vyuo vya kati na vikuu ili kutoa elimu ya lishe sahihi kwa kuanzisha klabu.
Akizungumza na Mwananchi Machi mwaka huu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alisema mkoa huo una wakazi 1,192,728 na asilimia 60 ni kundi la vijana, na asilimia 35 ni vijana waliopo katika rika balehe.
Anasema lishe huanzia ngazi ya familia tangu mtoto anapokuwa tumboni mpaka siku 1,000 za kwanza mpaka miaka mitano, kuanzia hapo hadi anakuwa mtu mzima (miaka 18) wengi wanakuwa katika eneo la shule.
“Shule inatumika kama nyenzo iwapo mtoto alikosa lishe nyumbani, hivyo tunatekeleza agizo la Serikali kuhakikisha watoto kwenye shule zetu zote wanapata angalau mlo mmoja kamili na utekelezaji umefikia karibu asilimia 98 kwa shule za msingi na sekondari,” anasema.
Dendego ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, anasema mikakati iliyokuwapo ni kuwa na bustani ndogondogo za shule, kama shamba darasa na humo huzalisha chakula kwa ajili ya lishe.
Anasema Shule ya Sekondari ya Wasichana Iringa ni miongoni mwa zinazotekeleza mkakati huo.
Shule ya Sekondari ya Wasichana Iringa imezungukwa na miti ya matunda yakiwamo mapera na mapeasi, ikiwa na eneo kubwa lenye bustani za mbogamboga na viazi vikuu.
Matunda na vyakula hivyo vimekuwa vikitumiwa na wanafunzi kuboresha mlo. Dada Mkuu, Cecilia Kikoti mwanafunzi wa kidato cha tano shuleni hapo, anasema wameanzishiwa mradi wa bustani unaosimamiwa na walimu.
“Kazi za shambani zinafanywa na wanafunzi na msimu wa kiangazi tunamwagilia maji. Wanafunzi wanajifunza kulima na namna ya kuanzisha bustani, na umuhimu wa matunda na mbogamboga,” anasema.
Mwalimu wa chakula shuleni hapo, Dosca Costa anasema kila mwanafunzi ana tuta lake na kila mwaka hubadilishiwa aina ya kilimo cha mboga, viazi vikuu au zao lingine katika uzalishaji.
Mkuu wa shule hiyo, Lulu Ngatumbura anasema shule hiyo kongwe ina wanafunzi 912 wa bweni na kila mwezi Serikali hupeleka fedha ya chakula.
“Kazi yetu ni kusimamia kutokana na miongozo iliyowekwa na Serikali kuhusu lishe na viwango vyake,” anasema.
Ngatumbura anasema kuna klabu ya lishe shuleni hapo ambayo watoto hushiriki kuhakikisha wanatengeneza lishe yao, kwa kulima na kutunza bustani.
Anasema awali mbogamboga na matunda walikuwa wakipata kutoka kwa wazabuni lakini anasema havikuwa na ubora.
“Tuliona ni vema tuzalishe mboga wenyewe na kudhibiti kile kinachokuwepo, watoto wanahusika moja kwa moja kwenye kulima, kuvuna hadi kinapokwenda jikoni,” anasema.
“Kwa mtindo huo watoto wanapata pia uzoefu maana tunalima spinachi, kabeji, vitunguu, viazi vitamu, maharage, sukuma wiki na mchanganyiko wa mbogamboga,” anasema.
Ngatumbura anasema wanafunzi hawashiriki kupiga dawa kwa kuwa kuna walimu maalumu wanaoshughulika na suala hilo.
Anasema katika kukamilisha mlo wenye virutubisho wanatumia unga wa mahindi lishe kwa ajili ya uji kwa sababu kuyapata kwa wingi siyo rahisi, lakini pia unga wanaotumia kwa ugali umeongezwa virutubisho, vivyo hivyo kwa mafuta, maharage na chumvi.
Imeandikwa kwa ushirikiano na Bill & Melinda Gates Foundations