Sumbawanga/Mbeya. Ndugu wawili wa familia moja kutoka ukoo wa Kapufi, Jofrey Dominiko na Elasto Dominiko, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumuua Charles Mwanazumi katika mgogoro wa kugombea shamba.
Mauaji hayo yalifanyika Desemba 10, 2020 katika Kijiji cha Sandula Wilaya ya Sumbawanga huku mwanaye Annek Mwanazumi akishuhudia, wakati alipokuwa shambani na baba yake eneo la Mchese kijijini hapo.
Wakati ndugu hao wakihukumiwa kunyongwa, ndugu wengine wawili wa ukoo mmoja, Abel Mwangoka na Watson Mwangoka waliokuwa wakituhumiwa kumuua mwanaukoo mwenzao, Hadson Mwangoka, wameachiwa huru na Mahakama.
Hukumu ya kunyongwa ilitolewa Mei 23, 2024 na Jaji Deo Nangela wa Mahakama Kuu Sumbawanga mkoani Rukwa wakati ile ya kuwaachia huru washitakiwa wawili ilitolewa Mei 24, 2024 na Jaji Mussa Pomo wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya.
Katika hukumu yake, Jaji Nangela alisema baada ya kuchambua ushahidi, ameshawishika kuwa mgogoro wa ardhi ni kisababishi kilichochochea washitakiwa kwenda kumshambulia Mwanazumi na kusababisha kifo chake.
Jaji alisema kwa msingi huo na kwa kuzingatia silaha zilizotumika, ukatili wa shambulizi lenyewe na sehemu za mwili zilizoshambuliwa, yote hayo yanatosha kuthibitisha nia ovu ambayo imewatia hatiani washitakiwa.
Jaji alisema sio tu kwamba washitakiwa walishiriki kumshambulia Charles Mwananzumi na kusababisha kifo chake, bali walifanya hivyo kwa nia ovu na kulikuwa hakuna uhalali wowote wa kuhalalisha mauaji hayo ya kikatili.
“Kwa kuegemea uchambuzi wa ushahidi, Mahakama inahitimisha kuwa washitakiwa hawa wawili wana hatia ya kosa waliloshitakiwa nalo,”alisema Jaji Nangela na kusema adhabu ya kosa hilo ni moja tu, nayo ni adhabu ya kifo.
Jamhuri na kiini cha mauaji
Washitakiwa katika kesi hiyo ni wana familia kutoka ukoo wa Kapufi Kijiji cha Sandula; marehemu alikuwa akitokea ukoo wa Mwananzumi, akiishi Kijiji cha Jirani cha Kalole ambacho hakiko mbali na Kijiji cha Sandula.
Maelezo ya upande wa mashitaka ni kuwa kabla ya tukio la mauaji kutendeka, koo hizo mbili zilikuwa katika mgogoro wa kipande cha shamba kilichopo Sandula, kutokana na mgogoro huo, marehemu alisitisha kulima hapo tangu mwaka 2016.
Aliamua kukodi shamba kutoka kwa Didas Mirambo na tangu wakati huo alikuwa akilima katika shamba hilo na alitakiwa kumkabidhi mmiliki wake mwaka 2023 kwa kuwa ndio makubaliano yao yalikuwa yanafikia mwisho.
Ilidaiwa kuwa Desemba 10,2020, alikuwa katika shamba hilo pamoja na mwanaye wa kiume, Annek na Method Mangulu na walikwenda shambani hapo tangu saa 1:00 asubuhi kwa ajili ya kufanya shughuliza zao za kilimo.
Wakati wakiendelea na shughuli hiyo, washitakiwa hao wawili wakiwa na ndugu zao wengine sita, ambao hawakupatikana, wakiwa na mapanga, mashoka, fimbo na nondo walifika shambani hapo na kuanza kumshambulia Charles Mwanazumi.
Kutokana na mashambulizi hayo, walimwacha akiwa amejeruhiwa vibaya huku Method Mangulu akijeruhiwa mguuni.
Baada ya kumaliza kufanya ukatili huo, washitakiwa na washirika wao walitoroka kutoka eneo la tukio na kutokomea kusikojulikana lakini wasilolijua, ni kuwa kwa mbali kidogo alikuwepo Arnold Mwanazumi aliyeshuhudia mauaji hayo.
Huyo ndiye alikuja kutoa msaada na kumchukua Charles kumwahisha Kituo cha Afya cha Kaengesa lakini hata hivyo ilipofika jioni ya siku hiyo, majeruhi huyo alifariki dunia wakati madaktari wakiendelea na jitihada za kuokoa uhai wake.
Tukio hilo liliripotiwa kituo cha Polisi cha Laela ambacho kilianzisha uchunguzi na Desemba 12,2020, polisi walifanikiwa kumkamata mshitakiwa wa kwanza, Jofrey na Desemba 20,2020 wakafanikiwa kumkamata mshitakiwa wa pili, Elasto.
Mashahidi walioshuhudia mauaji
Katika Ushahidi wake, Annek Mwanazumi ambaye ni mtoto wa kiume wa marehemu, alisimulia namna walivyofika shambani asubuhi hiyo na baba yake kushambuliwa kwa mapanga na kundi la watu ambao hakuweza kushika sura zao.
Ingawa hakuweza kuwakariri sura, lakini aliieleza mahakama kuwa ni baba yake akiwa anaugumia maumivu ndiye aliyemweleza kuwa ni mshitakiwa wa kwanza na ndugu zake ndio waliomshabulia na kwamba Arnold ndiye aliyetoa msaada.
Katika ushahidi wake, Arnold Mwanazumi ambaye ni kaka wa marehemu alisema siku ya mauaji, yeye alikuwa akijishughulisha na kilimo shambani kwake katika eneo la Vinyimbo, umbali wa kama meta 50 kutoka alipokuwa marehemu.
Alieleza kuwa kwenye saa 1:00 asubuhi kulikuwa na mgogoro na alisikia kundi la watu wakisema “mkamateni, mshike” aliona kundi la watu wakimshambulia mdogo wake na aliweza kuwatambua watano kati yao.
Aliwataja aliowatambua kuwa ni washitakiwa hao wawili na kwamba wauaji wa mdogo wake walitumia muda wa kama dakika 10 na yeye alikuwa upande wa pili wa mto unaotenganisha eneo la Chezya na Mchese.
Aliieleza Mahakama kuwa yeye ndio alimchukua mdogo wake na kumuwahisha kituo cha Afya cha Kaengesa ambako alifariki dunia na tukio hilo liliripotiwa kituo kidogo cha polisi cha Kaengesa na baadae Kituo cha Polisi cha Sumbawanga.
Washitakiwa hao walipapata nafasi ya kujitetea walikanusha tuhuma hizo na mshitakiwa wa kwanza Jofrey alikiri kuwa kabla ya kukamatwa kwake, kulikuwa na mgogoro wa ardhi kati ya ukoo wa Nemes Mwananzumi na ukoo wa Kapufi.
Kwa upande wake, mshitakiwa wa pili, Elasto Dominiko, alikanusha tuhuma hizo na kueleza kuwa anatambua uwepo wa mgogoro baina ya koo hizo mbili na kukanusha kuwa alionekana eneo la tukio akisema alikuwa kijijini Sandula.
Wawili waachiwa huru Mbeya
Katika hukumu yake, Jaji Mussa Pomo wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya, aliwaachia huru washitakiwa wawili wa mauaji, Abel Mwangoka na Watson Mwangoka, akisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka hilo.
Jaji alisema katika ushahidi wote uliotolewa, hakuna shahidi hata mmoja wa upande wa mashitaka ambao waliwashuhudia washitakiwa au mtu mwingine yeyote akifanya kitendo ambacho kilisababisha kifo cha Hadson Mwangoka.
Mauaji hayo yalitokea Machi 11,2010 katika Kijiji cha Shua Wilaya ya Mbeya.
Ushahidi wao uliegemea taarifa za kuambiwa baada ya marehemu kutoweka, baadaye mwili wake kubainika ukiwa umezikwa.