Wanne wadakwa kwa kusafirisha punda 46 nje ya nchi

Jeshi la Polisi kikosi cha kupambana na kuzuia wizi wa mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Longido mkoa wa Arusha limewakamata watuhumiwa wanne pamoja na mifugo aina ya punda 46 wakisafirishwa kinyume na taratibu kwenda nje ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yamebainishwa leo Jumamosi na Kamanda wa Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa Mifugo nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Simon Pasua wakati akizungumza na waandishi wa habari

Amesema majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na pindi upelelezi utakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa katika vyombo vya sheria kujibu tuhuma zao.

Kamanda Pasua amesema tayari serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi ilishatoa maelekezo juu ya katazo la kusafirisha punda na mazao yake kutokana na kupungua kwa idadi ya Wanyama hao.

Amesema Jeshi hilo litaendelea kuwakamata wale wote watakaobainika kuhusika na usafirishaji wa punda kwenda nje ya nchi.

Aidha, amebainisha kuwa Jeshi hilo litaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwakamata wale wote watakaokaidi agizo hilo la serikali.

Related Posts