Wanolewa bongo mtandao kwa vijana ukizinduliwa

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, mawaziri na wabunge wamewafunza vijana namna ya kujitambua na kupambania fursa za uchumi, uongozi na maisha.

Hayo yakifanyika, Serikali imetangaza kuanzisha vituo maalumu vya uatamizi kwa vijana.

Waliotoa mafunzo hayo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi; Waziri wa Madini, Antony Mavunde na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Wengine ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Ummy Ndeliananga na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma.

Mafunzo hayo wameyatoa leo Mei 25, 2024 wakati wa uzinduzi wa Mtandao wa Vijana wa Taifa Letu, Kesho Yetu (TK Movement) jijini Dodoma.

Mtandao huo unaowashirikisha vijana kutoka mikoa 32 nchini ni vuguvugu la vijana wanaoamini katika mapinduzi ya kifikra na kuwa mgawo sawa wa rasilimali ni haki ya kila raia.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Zungu amewataka vijana kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu ili kupata viongozi bora.

“Hamuwezi kupata viongozi bora kama hamtapiga kura na baada ya hapo tuingie kwenye kuboresha daftari la wapiga kura ya Rais na sisi (CCM) tulishaomba 2025 fomu ni moja tu ya Rais Samia,” amesema.

Amewataka vijana kwenda kumsemea Rais Samia mambo aliyoyafanya katika kipindi chake cha miaka mitatu ya uongozi ikiwemo miradi mikubwa iliyofanyika bila kusimama.

“Tunavyomsifia na kumpamba (Rais Samia) tunafanya hivyo kwa sababu anawatumikia Watanzania kwa dhati, kwa upenzi na kwa nguvu zote kuhakikisha Taifa linakwenda mbele…Tumpende mama (Rais), tuipende Tanzania kama tunavyovipenda vilabu vyetu (vya soka)” amesema.

Mwinjuma amewataka vijana kujifunza kutokana na historia ya maisha na kutokata tamaa, hata kama wanapitia changamoto.

Akisimulia historia yake, Mwinjuma amesema alishawahi kuacha viatu nyumbani na kwenda shuleni pekupeku kwa sababu alikuwa akihofia viatu vitachafuka.

“Sio uongo, nilishaenda shule bila viatu, nilishatoa funza kama ‘buku’. Ninachotaka kuwaambia haijalishi historia yako huko nyuma ilikuwaje, kuna mahali unafika una jukumu la kuibadilisha,” amesema.

Amewataka vijana kufungua macho na kuangalia Mungu alivyowapangia kuishi duniani kwa lengo la kujiendeleza.

Mwinjuma amesema kwa jinsi Rais anavyoiendesha Tanzania, kila mtu ana nafasi ya kufanikiwa kutokana na kusafishwa kwa nchi.

“Ingekuwa amri yangu, hata uchaguzi mwakani usingekuwepo moja kwa moja tungempa huyu mama (Rais Samia)… Tuna jukumu la kumrudisha mama madarakani,” amesema.

Ndejembi amesema kumekuwa na changamoto kubwa kwa vijana hasa wanapohitaji mikopo kwenye taasisi za kifedha, jambo ambalo linawarudisha nyuma.

“Wakati mwingine fremu za kufanyia biashara nazo ni tatizo, mtu hajaanza kazi yoyote anaambiwa awe na fremu ya biashara ambayo wamiliki wanataka kodi ya hadi miezi 12, hii si sawa,” amesema.

Amesema idadi ya vijana wanaohitimu vyuo vikuu ni zaidi ya 800,000 lakini wanaoingia soko la ajira ni asilimia tano tu.

Kwa mujibu wa Ndejembi, Serikali imeweka mazingira bora ya kuwawezesha vijana kuwa wajasiriamali kwa kuwa na vituo atamizi katika mikoa yote nchini.

Amesema vituo hivyo vitatumiwa na vijana wenye mawazo mazuri ya ujasiriamali, ambao watakwenda kwa ajili ya kuanzisha biashara bila kujali gharama za kodi ya pango na nyingine.

Ndejembi amewataka wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa mitaa na vijiji, pamoja na taasisi mbalimbali wawape vijana ushirikiano wa kutosha wanapopita kwenye maeneo hayo.

Bashe amesema kundi hilo litakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa likitumiwa na kupewa ushirikiano kutoka kwa viongozi.

Amesema kinachowaunganisha vijana ni utaifa wao, uzalendo na kujitolea, hivyo washirikiane katika fursa zinazotolewa na Serikali maeneo yote.

Amewataka vijana kutogeuza fursa na kujinufaisha wenyewe hasa baada ya kupewa dhamana ya kuwaongoza wenzao kwenye maeneo yao.

Mbunge wa Buchosa, Erick Shigongo amesema ni wakati wa kuwaambia ukweli vijana kwamba wasome kwa bidii, kuwa na maarifa lakini wasitegemee kwamba kuna ajira.

Shigongo amesema bado watu wanasoma kwa kutegemea kuajiriwa wakati hakuna ajira mtaani, lakini wakielezwa ukweli wanakuwa na uhakika wa kujua baada ya masomo wanakwenda kufanya nini.

Related Posts