Wawakilishi wataka ukarabati wa shule kongwe

Unguja. Licha ya mafanikio ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kujenga shule mpya za kisasa, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema kuna haja ya kuzifanyia ukarabati mkubwa za zamani ili kuleta usawa kwa wanafunzi.

Pia wameitaka wizara kutoa ufafanuzi kuhusu miongozo wanayotumia kuita majina shule zinazojengwa,  kwani huenda majina ya asili yakapotea kutokana na mabadiliko wanayofanya na vizazi vijavyo kushindwa kuelewa historia ya maeneo yao.

Wakichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 katika Baraza la Wawakilishi, linaloendelea Chukwani mjini hapa, wamesema zipo shule ambazo zinatia aibu kwa uchakavu.

Mwakilishi wa Mwera, Mihayo Juma Nhunga, akichangia mjadala Mei 24, 2024 amesema pamoja na kujengwa shule za ghorofa, bado zipo ambazo ni chakavu kupita kiasi, hata sare za shule za wanafunzi zinabadilika rangi kutokana na mazingira hayo.

“Zipo shule zimejengwa sawa, lakini haileti maana unakuta shule nzuri imejengwa  pembeni yake kuna ya zamani ambayo hata mwanafunzi akivaa sare ya shule siku moja hawezi kuirejea kutokana na kuchafuka, kwa mtindo huu hatuwezi kufika,” amesema.

Nhunga amesema viongozi wa wizara wamekuwa na utaratibu wa kutotekeleza ahadi wanazotoa barazani badala yake wanarejea zilezile kila bajeti, akiwataka wabadilike na kutekeleza wanayoahidi.

“Twende tukatende wananchi waone tutaisaidia Serikali katika utendaji kazi siyo maneno yetu,” amesema.

Katika hatua nyingine ametaka kupata maelezo ya wizara inatumia miongozo gani zinapojengwa shule, kwani zimekuwa zikibadilishwa majina na kuacha ya asili jambo ambalo linaweza kupoteza uhalisia kwa vizazi vijavyo akieleza majina hayo yana umuhimu wake.

“Kumekuwa na utaratibu wa kubadilisha majina bila sababu, haya ya asili yana maana yake, kila inapojengwa inabadilishwa yanawekwa mengine ambayo hayana uasilia, hili nalo ni hatari kwa vizazi vijavyo, vitashindwa kuelewa,” amehoji.

Mwakilishi makundi maalumu (Vijana), Hudhaima Mbarak Tahir amesema ipo haja kwa wizara kuongeza ubunifu na kuvisaidia vyuo vikuu kupata intaneti ya uhakika, kwani wanafunzi wanapata shida.

“Chuoni siyo chaki kusimama ubaoni, kinachotakiwa ni intaneti, lakini kwa sasa hali ilivyo huko vyuoni inatisha, mtandao ni shida gharama kubwa, elimu yetu tunaipeleka wapi kwa mtindo huu,” amehoji.

Pia alizungumzia kupungua bajeti ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Sh29 bilioni mwaka 2023/24 na kufikia Sh27 bilioni ya mwaka 2024/25 ilhali wanufaika wa mikopo wanaongezeka.

Amesema wapo wanafunzi wengi wanaotaka mikopo na ufaulu unaongezeka lakini haiingii akilini bajeti ya mikopo kupunguzwa.

Mwakilishi wa Gando, Mariam Than Juma amesema ipo haja ya kuweka wazi na kubainisha shule ambazo wanapanga kuzifanyia ukarabati.

Ameshauri kuangaliwa zaidi zilizopo visiwani kwani zimekuwa zikisahaulika badala yake kuangaliwa maeneo ya mijini.

Mjadala wa bajeti wa wizara hiyo utaendelea Jumatatu Mei 27, 2024 kwa wawakilishi kuendelea kutoa michango yao kisha waziri atafanya majumuisho kabla ya kupitishwa.

Related Posts