Baraza la Madiwani Mtwara Mikindani labatilisha umiliki ardhi ya mbunge

Mtwara. Baraza la Madiwani Manispaa ya Mtwara Mikindani, limebatilisha uhalali wa umiliki wa kiwanja katika eneo la Shangani Mashariki linalotajwa kumilikiwa na mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga baada ya kamati ya kudumu ya mipango miji, ardhi na ujenzi kujiridhisha kuwa eneo hilo ni mali ya halmashauri hiyo.

Akitoa maagizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Hassan Nyange kupitia Baraza la Madiwani, Meya wa Manispaa hiyo, Shadida Ndile amesema maeneo yote ya halmashauri yatambulike na kuwekewa alama ili kuzuia uvamizi.

Amesema yapo maeneo makubwa ya Manispaa lakini hayatambuliki, hivyo kusababisha watu kuvamia na kuleta taharuki,  huku akionya watendaji wa mitaa kutohusika na uuzaji wa viwanja bila kufuata utaratibu wa kisheria.

“Vipo viwanja ambavyo vimemilikishwa kwa watu binafsi pasipo utaratibu, ndiyo maana Baraza la Madiwani limeamua hati zirudi mara moja ni muhimu kuyatambua maeneo hayo na kuyawekea alama,” amesema Ndile.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mipango Miji, Ardhi na Ujenzi ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ambae pia ni diwani wa kata ya Naliendele, Masudi Dali,  amesema baada ya kupitia katika vikao vya kamati juu ya uhalali na historia, waligundua kuwa mmiliki wa eneo hilo hajafuata utaratibu wa umiliki.

“Unajua kile kiwanja cha Shangani ni mali ya manispaa ambapo amemilikishwa mbunge wa Mtwara mjini kinyume cha utaratibu baada ya kamati kujiridhisha kuwa ni mali ya halmashauri, Baraza limedhia eneo lirudi kwa halmshauri na kubatilisha hati,” amesema Dali.

Naye diwani wa kata ya Vigaeni Manispaa ya Mtwara Mikindani, Said Ali Nassoro (White) amesema halmashuri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ilipima eneo la Shangani miaka ya 1980 ambapo eneo hilo liliachwa kwa ajili ya matumizi ya Serikali na sio mtu binafsi.

Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga amesema eneo hilo awali lilimilikiwa na babu yake, alikuwa mmiliki wa asili ndiyo maana hata kokoto walikuwa wanachimba katika maeneo hayo hata ukienda utakuta mashimo makubwa.

Amesema katika eneo hilo kuna maeneo matatu; la kanisa, la kwake na la mtu mwingine, hakuna eneo la halmashauri na kama walichukua eneo, aliuliza ni nani  waliyempa fidia.

“Awali, eneo hilo hapakuwa na mchoro wowote na halijawahi kupimwa wala watu kupewa fidia, tunajua maeneo ambayo yanarasimishwa watu wanalipwa fidia, lakini halmashauri haikufanya hivyo, ndiyo maana nilipimiwa na ardhi tukaanza michoro upya,” amesema Mtenga. 

“Mimi namiliki eneo hili kisheria, nimepata hati kisheria nilifuata utaratibu na pia nilianzia kwa mwenyekiti wa serikali za mitaa wakakaa kwenye kamati wakanitambulisha kwa mkurugenzi nikapewa barua, nikaenda kuapa mahakamani wakaweka na bango ili kama eneo lina mgogoro wajitokeze, lakini hakuna mtu aliyejitokeza,” amesema Mtenga.

Ameongeza: “Wapo baadhi ya madiwani wanapeleka watu katika maeneo yale kutaka kuwauzia na mwingine alifunga safari kuja Dodoma, akataka nimuhonge Sh10 milioni ili kumnyamazisha, nikakataa kwa kuwa eneo hilo halijawahi kupimwa wala kumilikiwa na halmshauri, walivyo na uchu hata jana kapelekwa mtu kuonyeshwa eneo ili wamuuzie eneo langu kisa wamefuta umiliki. Baraza la Madiwani halina mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi.”

Related Posts