Dar es Salaam. Hofu ya kukamilika kwa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) inaendelea kupata mashiko, kufuatia kuendelea kushuhudiwa kwa ahadi zisizotimizwa za kukamilishwa utekelezwaji wa vipande mbalimbali vya ujenzi huo.
Sambamba na ahadi zisizotimizwa, Mwananchi imeshuhudia wafanyakazi katika kambi mbalimbali wakiondolewa na mkandarasi kwa kile kinachodaiwa kuwa Serikali haina fedha ya kumlipa kuendelea na kazi.
Ukurasa wa ahadi zilizo za kweli, ulifunguliwa katika utekelezwaji wa kipande cha kwanza cha mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, kilichotakiwa kukamilika kwa miezi 30, lakini ilishindikana na kuongezewa miezi 18.
Ukiachana na ahadi hiyo na nyingine nyingi, kipande cha tano cha Isaka-Mwanza kilichopaswa kukamilika Mei 14, mwaka huu nacho kimevuka muda wa mkataba. Ni siku nne zimesalia kufunga mwezi huu, lakini utekelezaji wake haujafikia hata asilimia 80.
Kamati ilivyoonyesha shaka
Shaka ya kukamilika kwa ahadi ya utekelezwaji wa kipande cha Isaka-Mwanza, ilionyeshwa hata na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundimbonu.
Katika taarifa yake bungeni jijini Dodoma Aprili 6, 2024, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso, alishuku iwapo kipande hicho cha mradi wa SGR kitakamilika kwa wakati.
Msingi wa shaka yake ni kukaribia kwa siku inayopaswa kuwa mwisho wa mradi, ambayo ni Mei 14, mwaka huu lakini hatua za utekelezaji zikiwa katika asilimia 54.01.
Mbali na shaka hiyo, katika taarifa ya kamati siku hiyo ambayo Bunge lilijadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya uchukuzi kwa mwaka 2024/25, kamati hiyo ilieleza Serikali imeshamlipa mkandarasi Sh1.343 trilioni, sawa na asilimia 40.53 ya gharama ya mradi.
“Kamati ina shaka kuhusu muda uliobaki kukamilisha mradi husika kufikia Mei, 2024 ukilinganisha na asilimia iliyobaki ya ujenzi.
“Serikali ilitaarifu Kamati kwamba, wana matumaini kuwa mkandarasi atakamilisha ujenzi kwa sababu kazi iliyobaki sio kubwa ukilinganisha na kazi iliyofanyika tayari,” alisema.
Hata hivyo, tayari tarehe iliyopangwa kwa ajili ya mradi huo kukamilika imeshapita na Mwananchi limebaini kuwa kazi hazijaisha.
Kwa mujibu wa Kakoso, kamati katika taarifa yake, imebaini kuwepo kwa malalamiko ya wananchi, kutokana na kutolipwa fidia baada ya maeneo yao kutwaliwa kupisha mradi.Alipendekeza Serikali ifanikishe malipo ya wananchi hao kwa mujibu wa sheria.
Danadana za kuchelewa kwa mradi huo pamoja na mingine ya SGR, kunahusishwa na changamoto za kifedha ambazo Serikali inadawa kushindwa kumlipa mkandarasi CCECC kutoka Jamhuri ya Watu wa China, akamilishe kazi hiyo.
Hilo, linathibitishwa na baadhi ya wafanyakazi katika kambi mbalimbali za mradi huo, wanaolalamikia kuondolewa kazini kwa kile walichoambiwa na mkandarasi, Serikali haina fedha za kulipa ili mradi uendelee.
Mmoja wa wanaofanyakazi katika mradi huo kipande cha Isaka-Mwanza (jina lake limehifadhiwa), alisema katika kambi yao walianza wakiwa wafanyakazi zaidi ya 400 lakini waliosalia sasa ni 50.
Katika kambi hiyo ya Luvumbo, mfanyakazi huyo alisema upunguzaji wa wafanyakazi ulianza Aprili 20, 2024 walipopunguzwa watu zaidi ya 100.
Kwa mujibu wa mfanyakazi huyo, upunguzaji uliendelea hadi kumfikia yeye na sasa wamesalia wafanyakazi 50 katika kambi hiyo.
“Sisi tulipunguzwa Ijumaa (Mei 24) waliobaki ni kama wafanyakazi 50 hivi na hata magari yameanza kuondolewa kuna dalili kwamba mradi umekwama,” ameeleza.
Sababu ya kupunguzwa kwao ni kile alichoeleza, wamearifiwa na idara ya rasilimali watu kuwa, kuna changamoto za kifedha zinazofanya washindwe kulipwa.
“HR (ofisa rasilimali watu) alipita na kutuambia kwamba Serikali haina fedha ya kumlipa mkandarasi aendelee na kazi, kwa hiyo tumetakiwa kwenda nyumbani kwa mwezi mmoja kisha wameahidi wataturudisha,” amesema.
Kuhusu malipo ya kusitishiwa mikataba, alieleza kwa waliokuwa na mikataba ya matazamio yaani miezi mitatu, mkandarasi ameahidi kuwalipa siku nne za ziada.
Lakini kwa wale waliokuwa wameshafanyakazi kwa zaidi ya miezi sita, alisema wanalipwa hela ya likizo ya mwaka mmoja kwa hesabu ya Sh16,600 kila siku.
Ameeleza hatua hiyo ni pigo kwake, kwani imetokea ghafla, ingawa wengine wapo kambini yeye ameamua kuondoka kwa kukosa fedha za kujigharimia.
Katika kutafuta ukweli wa hayo, Mwananchi iliwasiliana kwa simu na Meneja Rasilimali watu wa kampuni ya Yepi Merkez aliyegoma kutaja jina lake, alielekeza atafutwe msemaji, kwani si mamlaka yake kuzungumzia kampuni.
“Siwezi kuzungumzia hilo mtafute mtu wa mawasiliano au meneja mradi,”amesema.
Hata alipotafutwa msemaji huyo, simu yake iliita bila majibu.
Hata hivyo, meneja wa mradi huo alipotafutwa naye alidai tayari alishaondoka kabla ya barua kusambazwa kwa wafanyakazi wengine.
Mkutopora-Tabora nao hali tete
Wengine waliokumbwa na kadhia hiyo ni wale wanaofanya kazi katika kipande cha Makutopora hadi Tabora chenye urefu wa kilomita 368.
Kwa mujibu wa mmoja wa wafanyakazi hao, waliarifiwa hakutakuwa na kazi katika eneo hilo hadi pale watakapopigiwa simu na kwamba tangu Septemba mwaka jana zaidi ya watu 1,000 wamepunguzwa.
Kipande hicho cha SGR kinachotekelezwa na mkandarasi Yapi Merkezi, mfanyakazi huyo anadai sababu ya kupunguzwa kwao ni Serikali kukosa fedha ya kumlipa mkandarasi.
Tangazo la Yapi Merkezi lililotolewa Mei 23, 2024 liliwaelekeza wafanyakazi wote likisema:
“Kuanzia Mei 23/2024 hakutakuwa na kazi hadi mtakapoarifiwa na idara ya rasilimali watu na wakuu wa idara husika kurudi kazini. Tafadhali hakikisha simu yako inapatikana muda wote.”
Mfanyakazi huyo amesisitiza mkandarasi amewaarifu hana fedha kwa sababu mwajiri wake (Serikali), imeishiwa.
“Yapi Merkezi wametuambia hawana fedha Serikali imeishiwa hela ya kuendelea na mradi, hali si nzuri miradi mingi nimewasiliana na wenzangu inasuasua hivyo watu wengi wamerudishwa nyumbani, mimi nimesimamishwa kuanzia Februari,” amesema.
Mfanyakazi mwingine katika mradi huo, alisema ameona tangazo hilo katika kipindi ambacho tayari alishaondolewa kazini tangu Februari 2024.
“Tunaomba Serikali imlipe Yapi Merkezi hatuna kazi za kufanya mimi nipo nyumbani tu, nimeambiwa nitapigiwa simu lakini sijui nini kitatokea huenda ndio mwisho wa ajira zetu,” amesema.
Kipande hicho cha Makutupora-Tabora kinagharimu Sh4.606 trilioni na matarajio ya kukamilika kwake ni ndani ya miezi 42 kuanzia Aprili mwaka 2022.
Serikali yaahidi kuendelea na kazi
Pamoja na kuwepo kwa uhalisia huo, katika hotuba yake ya Mei 6, 2024, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi huo kwa awamu zote mbili zenye jumla ya mtandao wa kilomita 2,809.
Sambamba na awamu hizo, waziri huyo alisema Serikali itaendelea na ujenzi wa reli hiyo kwa maeneo mengine ya Ushoroba wa Kusini na Kaskazini kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha.
Katika mazungumzo yake hayo, Profesa Mbarawa alisema utafutaji wa fedha kutoka kwa wadau unaendelea, wakiwemo wawekezaji kwa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Ushirikiano huo, kwa mujibu wa Mbarawa unalenga kufanikisha ujenzi wa reli hiyo kwa maeneo yaliyobaki yanayojumuisha kutoka Kaliua – Mpanda – Karema (kilomita 321), Isaka – Rusumo – Rwanda (kilomita 371), Mtwara – Mbambabay na matawi ya Liganga na Mchuchuma (kilomita 1,000).
Vipande vingine ni Tanga – Arusha – Musoma (kilomita 1,028), Reli ya Jiji la Dar es Salaam (kilomita 166) na Reli ya Jiji la Dodoma (kilomita 107).
Alieleza mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji wa miradi ya uchukuzi kuhitaji fedha nyingi (capital intensive) katika utekelezaji wake. Mathalan,Mradi wa SGR utagharimu takriban Shilingi trilioni 23 hadi kukamilika kwake.
Ukiachana na maelezo yake ya Mei 6, mwaka huu,Mwananchi kwa siku za karibuni limekuwa linamtafuta Profesa Mbarawa azungumzie madai yote, simu yake iliita bila majibu.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi na kwa njia ya WhatsApp ilionyesha umefika, lakini haukujibiwa.
Pamoja naye, alitafutwa pia Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Godius Kahyarara, alipokea na kudai yuko kikaoni na kwamba angepiga simu baada ya kutoka.
Hadi habari hii inamaliza kuchapwa mtendaji mkuu huyo wa wizara hiyo hakumtafuta tena mwandishi na hata alipotafutwa simu yake iliita bila kupokelewa.