Dar es Salaam. “Kwa sasa nina miaka 33, lakini siwezi kusahau kitendo nilichofanyiwa na kaka yangu nikiwa na miaka 11.
“Hakuwa kaka yangu wa kuzaliwa naye tumbo moja, bali mtoto wa mama mkubwa, hivyo tuliishi nyumba moja kama watoto wa familia moja. Sijui kitu gani kilimuingia akanibaka na iligundulika kuwa amefanya kitendo hicho, lakini ikaamuliwa ifanywe siri.
“Nilikuwa mdogo, lakini nakumbuka fika namna jitihada zilivyofanyika ili watu wasijue, hivyo ndivyo ilivyokuwa, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi leo yule kaka yupo anaendelea na maisha yake. Binafsi sikuwa na cha kufanya, ila kitu ambacho nina uhakika nacho mpaka sasa nina chuki kubwa dhidi yake, sijawahi kumsamehe, namchukia yeye na wote waliopambana kumlinda.”
Hayo ni maneno ya mmoja wa waathirika wa ubakaji ndani ya familia, binti huyu alikumbana na ukatili huo akiwa na umri mdogo, lakini maumivu yatokanayo na madhila aliyopitia hadi sasa bado yapo kichwani mwake.
Si huyo tu, msanii wa filamu nchini, Getrude Mwita ameshawahi kuweka wazi kuwa alinusurika kubakwa na mjomba wake, kitendo kilichomfanya atoroke nyumbani na kwenda kuishi mtaani.
Hayo ni baadhi ya matukio machache kati ya mengi ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto ambayo yanaendelea kushamiri kila uchwao.
Mwananchi imekusanya machache kati ya mengi yaliyotokea Aprili na Mei, mwaka huu.
Miongoni mwa matukio hayo ni lile lililomhusisha Stanley Mbena (39), anayedaiwa kumlawiti mtoto wake mwenye umri wa miaka tisa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza lilitokea Mei 3, mwaka huu katika eneo la Kilakala, Manispaa ya Morogoro.
Noela Barnabas, mama mzazi wa mtoto huyo amesema alitengana na mzazi mwenzake na akawaacha watoto kwa baba yao bila kujua anaweza kufanya vitendo vya ukatili.
“Nilianza kugundua mwanangu anafanyiwa vitendo hivyo vya ukatili mwishoni mwa mwaka jana nilipokwenda kuwachukua. Nilipokuwa naye nyumbani niliona uchafu unatoka kwenye njia ya haja kubwa, nilimweleza mzazi mwenzangu na aliniahidi atafuatilia, lakini hajafuatilia mpaka nilipopata taarifa kuwa yeye ndiye anatuhumiwa kufanya vitendo hivyo,” amedai Noela.
Pamoja na kugundua ukweli huo, mama huyu hakuchukua hatua kwa kuhofia kulaumiwa na familia, hata hivyo majirani walishughulikia suala hilo kwa kuwahusisha watu wa ustawi wa jamii, ndipo baba huyo alipokamatwa.
“Kwa sasa familia nzima ya yule mwanaume inaniona mbaya na wanasema nimechangia ndugu yao kupewa kesi. Hilo linanifanya niishi kwa mashaka na wasiwasi mkubwa. Nashukuru baada ya kufanyiwa vipimo, watoto wote nimeshakabidhiwa ninawalea mwenyewe,” amesema Noela.
Huko mkoani Njombe Jeshi la Polisi lilimkamata Barnabas Ndewe (32) kwa tuhuma za kumnajisi mtoto wake mwenye wa miaka 13.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mohamed Banga alisema tukio hilo lilitokea Aprili 14, 2024, baba huyo alipokwenda polisi kwa ajili ya kumshtaki kijana aliyeanzisha uhusiano na mtoto wake, lakini mtoto huyo akawaeleza polisi baba yake amekuwa akimnajisi.
Mtoto huyo alidai baba huyo amekuwa akimfanyia kitendo hicho tangu mwaka 2022.
Aprili 5, 2024 Jeshi la Polisi mkoani Mtwara lilitoa taarifa ya kukamatwa kwa Said Mapesa (42), akituhumiwa kumbaka na kumpa ujauzito mtoto wake wa kambo mwenye miaka 15.
Mtoto huyo alidai baba yake alikuwa akitekeleza ukatili huo muda ambao mama yake hayuko nyumbani na alikuwa akimtishia asimueleze mtu yeyote kitendo anachofanyiwa.
Tukio lingine ni lile lililotokea mkoani Mwanza, mkazi wa Nyakato, Bashiri Mohamed alifikishwa kizimbani kwa kosa la kuzini na mtoto wake wa kumzaa mwenye miaka 16.
Mohamed alifikishwa katika Mahakama ya Ilemela Mei 21, 2024 na kusomewa shtaka hilo analodaiwa kulitenda kati ya Septemba na Februari 15, 2024.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Serikali, Mwanahawa Changale, kosa hilo ni kinyume na kifungu namba 158 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.
Mwanasaikolojia Christian Bwaya anasema tafiti zinaonesha vitendo vingi vya ukatili kwa watoto hutekelezwa na watu wa karibu na mtoto.
Anasema tafsiri yake ni kwamba, watu ambao mtoto anawaamini zaidi, ndio hao wanaomgeuka na kumlawiti au kumbaka.
Bwaya anasema vitendo vya aina hiyo vikifanywa ndani ya familia vina athari kubwa, mtoto anajisikia kusalitiwa kwa kiwango kisichoweza kuelezeka katika umri mdogo.
“Tumesikia mifano ya baba kumlawiti mtoto wake mwenyewe wa kumzaa. Wapo wanaowabaka watoto wao wa kambo kwa sababu mbalimbali, ikiwepo kisasi kwa mzazi mwenzake.
Bwaya anasema inapotokea mtu wa karibu kama baba anambaka mwanaye kwa mfano, madhara makubwa ya ngazi tatu yanaweza kutokea kwa mtoto mwenyewe.
“Kwanza, mtoto hujifunza usaliti katika umri mdogo. Hakuna kitu kina madhara makubwa kwa mtoto kama kusalitiwa kwa kiwango kisichoweza kuelezeka kwa maneno. Fikiria unamwamini baba ukiamini huyu ndiye mtu wa kwanza kumkimbilia unapokuwa na shida. Kesho ndiye anakufanyia kitendo cha aibu kinachokuachia majeraha ya muda mrefu.
“Fikiria namna kitendo hicho kinavyoweza kuathiri mtazamo wako kuhusu wewe mwenyewe na familia. Katika mazingira kama haya, ni vigumu mtoto huyu kuja kumwamini mtu mwingine katika maisha yake.
Hata kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi inaweza kuwa safari ngumu kwa mtoto wa namna hii. Uwezekano wa kuogopa mapenzi ni mkubwa.
Pili, mwanasaikolojia huyo anabainisha, baba anayefanya vitendo hivi huficha aibu yake kwa kumtisha mtoto kuwa akithubutu kusema atamdhuru au mama yake.
“Kutishwa kwa kiwango hiki katika umri mdogo si jambo dogo. Vitisho hubadili mtazamo wa mtoto kuhusu maisha. Mtoto anayetishwa kuficha siri, hujenga woga na kumnyang’anya hali yake ya kujiamini. Kupoteza kujiamini ni kupoteza utu na thamani yako katika maisha.
“Huwezi kufikiri sawa sawa. Huwezi hata kujifunza vizuri. Maisha yanakuwa yameshaharibika. Kazi ya kuishi na siri kubwa inayotafuna maisha yako kimya kimya inaweza kukuingiza kwenye migogoro,” anasema na kuongeza:
“Mtoto ataishia kumchukia baba, lakini pia huwezi kuwaambia watu kuwa kuna kitu amekufanyia. Hali hii si tu huathiri mshikamano wa kifamilia, lakini inaweza kumuingiza kwenye chuki kubwa na watu wake wa karibu.”
Anasema mtoto asiye na muunganiko na familia yake anaweza kugeuka kuwa hatari kwa jamii.
Anasema ni kwa sababu anakuwa ni mtu aliyetawaliwa na visasi na chuki kichwani mwake.
Bwaya anasema mtoto anayepitia hali hiyo anakuwa hatarini kuingia kwenye changamoto ya afya ya akili.
“Tunawafahamu watoto wa namna hii huishi maisha ya upweke wasijue nani mwingine wa kumwambia. Hujikuta wakiathirika sana kisaikolojia na huishia kwenye magonjwa ya afya ya akili. Wasipopata msaada wanaweza kuwa kwenye hatari kubwa ya kukabiliana na sonona na hatimaye kujitoa uhai.
Hili linaelezwa pia na Daktari wa afya ya akili, Pascal Kang’iria, anasema kuna uwezekano mkubwa wa mtoto anayepitia ukatili wa aina hiyo kuathirika kisaikolojia na hujikuta yuko kwenye hatari ya kupata changamoto ya afya ya akili.
“Kwa kawaida mtoto anazaliwa akiwa hana chochote kichwani, kadiri anavyokua ndivyo anaingiza vitu. Ikitokea amekutana na vitendo vya ukatili vikiingia kwenye ubongo wake na kumbukumbu hiyo ikabaki, lazima itamletea athari.
Anasema mwingine anaweza kuendelea kuishi na picha hiyo mpaka atakapokuwa mtu mzima. Na kadiri anavyozidi kuelewa alichofanyiwa, ndivyo anavyoweza kuanza kujitenga na kupoteza hali ya kujiamini, taratibu anatengeneza tatizo la afya ya akili,” anasema Dk Kang’iria.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka anasema kuna haja ya kuwa na mkakati wa kuwa na jamii salama, kinyume na hapo kuna hatari ya kuwa na kizazi cha kundi kubwa la watu waliofanyiwa ukatili na watu wao wa karibu.
Anasema jamii pia inapaswa kuwekeza kwenye malezi kwa kuhakikisha watoto wanalelewa kwa misingi bora itakayosaidia kuwaepusha kuangukia upande usiofaa.
“Hali ni mbaya. Kama tunakuwa na mikakati ya kukuza uchumi, kuendeleza elimu, basi hatuna budi kuwa na mkakati wa kutengeneza jamii salama. Hatuwezi kuendelea kuishi katika mfumo huu ambao watoto wanafanyiwa ukatili na watu wanaopaswa kuwalinda.
“Ni muhimu suala la malezi likapewa kipaumbele, siku hizi watu hawalei, wanafuga, sasa mtoto ambaye hajalelewa unategemea akiwa mtu mzima ataweza kulea? Sasa hapa si ajabu kukutana na baba wasio na maadili ambao kwao hawaoni shida kuwaingilia watoto wao,” anasema Sheikh Mataka.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosteness anasema nguvu kubwa inapaswa kuwekwa ndani ya familia kwa kuingiza mafundisho yatakayowafanya wanafamilia kuwa na hofu ya Mungu.
Askofu Jackson, ambaye pia ni mdau katika vita dhidi ya ukatili kwa watoto, anasema ni muhimu pia watoto wakafundishwa jinsi ya kujitetea kwa kuwa wanaopaswa kuwatetea ndio wamegeuka kuwa watu hatari kwao.
“Ni wakati sasa tuone umuhimu wa kuwafundisha watoto jinsi ya kukabiliana na kujitetea wanapokutana na vitendo vya ukatili. Wafundishwe kuondoa hofu na wawe tayari kutoa taarifa hata wanapokutana na vitisho,” anasema askofu huyo.
Anasema kitu kingine muhimu, wanaobainika kufanya vitendo hivi wafikishwe kwenye vyombo husika na sheria ifuate mkondo wake.