RAISI wa Yanga, Injinia Hersi Said amewahakikishia mashabiki wa Yanga leo Jumapili kwenye sherehe za ubingwa za timu hiyo kuwa hakuna mchezaji muhimu hata mmoja katika kikosi chao ambaye ataondoka mwishoni mwa msimu.
Hersi amesema hayo kuzima uvumi wa nyota Stephane Aziz KI ambaye amekuwa akihusisha na vigogo mbalimbali wa soka ndani na nje ya Afrika kufuatia kiwango bora alichoonyesha akiwa na timu hiyo kuanzia katika Ligi ya Mabingwa Afrika hadi katika mashindano ya ndani.
Kigogo huyo amesema hayo baada ya kushukuru wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo kwa kazi kubwa ya kutwaa ubingwa wa 30 kwa timu hiyo huku akisisitiza kwamba haikuwa rahisi.
“Tunawaahidi tutaenda kuupigania ubingwa na kutaubulisha hapa (FA dhidi ya Azam), zaidi ya hapo tunajukumu kubwa la kujenga timu yetu, tunaenda kujenga timu bora kuliko msimu huu, tunaenda kusaini wachezaji bora zaidi,” amesema Hersi na kuongeza;
“Mungu akipenda tutarudi hapa mwakani tena kufurahia mafanio yetu kwa upande wa kimataifa tunataka kufanya zaidi ya kile ambacho kimefanyika mwaka huu.”
Katika kile ambacho Hersi amekisema alionekana wiki chache zilizopita akiwa DR Congo ambako alienda kufanya mazungumzo ya kusajili wachezaji wapya ikiwa ni mapendekezo ya kocha Miguel Gamondi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Gamondi miongoni mwa maeneo ambayo Yanga inayafanyia kazi ni pamoja na upande wa beki ya kushoto na safu ya ushambuliaji kwa kuongeza mtu wa nguvu ambaye atasaidiana kazi na Joseph Guede.
Katika sherehe hizo, baada ya kuzungumza kwa Hersi wakati Harmonize akitumbuiza kwa dakika chache alimuita Aziz Ki na kumweleza vile anatamani kuendelea kumuona Jangwani kwa miaka mingine ijayo.
Aziz akiwa na tabasamu usoni alionyesha vidole viwili juu ikiwa ni miaka mingine miwili ambayo ameripotiwa kuwa anaweza kusalia zaidi akiwa na timu hiyo.
Fundi huyo wa Burkinafaso, ana vita mbili mbele yake ya kwanza ni kuwania kiatu cha ufungaji bora akiwa na Feisal Salum wa Azam nyingine ni kuipa ubingwa timu hiyo upande wa FA katioka mechi itakayopigwa Juni 2 kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja.