Kutokana na hali ya maisha kubadilika na kufanya wazazi wote wawili, yaani baba na mama kulazimika kufanya kazi au kwenda kazini, jukumu la malezi ya watoto majumbani limebakia kwa kiasi kikubwa mikononi mwa wafanyakazi wa ndani, maarufu kama “house girls”.
Jambo hili siyo tu limepunguza kwa kiasi kikubwa ukaribu wa watoto na wazazi wao, bali pia limeongeza kasi ya athari hasi katika mabadiliko ya tabia za watoto hawa na pia kuongeza hofu katika namna wanavyoishi na wafanyakazi hawa.
Wapo wazazi wanaoelezea mazingira ya watoto wao kutopewa chakula kama inavyopaswa, wapo wanaolalamika watoto wao kunyanyasika, wapo wanaolalamika kuhusu wadada hawa kuingiza ndani wapenzi wao wa kiume na hata kufanya nao ngono mbele ya macho ya watoto hawa wadogo, wapo pia wanaolalamika kuhusu tabia za kishirikina za wadada hawa.
Hii haiondoi ukweli kwamba wapo waliobahatika kuwa na wadada wenye tabia nzuri na wanaowapenda na kuwajali sana watoto, ingawa hili ni kundi dogo sana la wazazi kwa jumla.
Labda nizungumzie zaidi suala la wadada wa kazi kuwatesa na kuwanyanyasa watoto wetu, hususan kufuatia kuzagaa kwa video ya dada wa kazi aliyemtesa sana mtoto mdogo nchini Uganda, video ambayo imeangaliwa na mamilioni ya watu kupitia mitandao ya kijamii.
Inasemekana video hii imeangaliwa na watu zaidi ya milioni 20 kwa muda wa siku 5 tu. Hii itakuonyesha ni kwa jinsi gani watu wengi wameguswa na kuhamaki hali hii.
Swali ni je, haya mambo nyumbani kwako hayatokei? Na kama yamewahi kutokea, je, ni kwa kiasi gani? Na kama hayatokei, je, ni yapi mengine yanayotokea? Labda maswali haya yatatufungua macho na kutufanya kuwa waangalifu zaidi
Inabidi wazazi kufahamu kuwa wafanyakazi tunaowaajiri wanatoka katika mazingira tofauti tofauti na kwa jinsi wengine walivyokuzwa, kunyanyasika au kuonewa au kunyimwa haki labda hadi ndoto zao kukatishwa wakajikuta wanakuwa wafanyakazi wa ndani, tofauti na walivyotamani, ndivyo mianya ya hasira, visasi na machungu hupanuka na kuishia kwa watoto wetu wapenzi tuliowaacha wakae nao nyumbani.
Huku ukidhani kuwa mwanao yuko salama, kumbe yuko kwenye mikono ya muhanga wa maisha ya awali ambaye anaishi chini ya dari yako ili tu ale, alale na apate hela kidogo ya kujikimu, lakini moyoni mwake yamkini mazingira yameshamuandaa kuwa jitu na siyo mtu.
Ni vema tukafahamu historia za dada na kaka tunaowaajiri na kuishi nao chini ya dari moja.
Unaweza kumuuliza katika maongezi ya kawaida tu, fahamu hali ya familia yake, fahamu yeye ni wa ngapi kwao, fahamu mtazamo wake kwa watoto na katika kazi, fahamu amewahi kufanya kazi maeneo gani na hali ilikuwaje huko? Fahamu maisha na changamoto alizowahi kuzipitia maishani.
Jifunze kuwafanya wafanyakazi hawa wawe marafiki ili waweze kuelezea matukio yaliyowahi kuwasibu maishani mwao.
Usimuangalie tu dada huyu kama mfanyakazi kwa sababu unamlipa kamshahara, bali muangalie kama mtu anayekaa na watoto wako, tena anayekaa nao muda mrefu kuliko hata wewe, muangalie kama mtu uliyemuamini kwa maisha ya wanao au hata maisha yenu wote kwa sababu yeye mara nyingine ndio mpishi wa chakula chenu.
Watu hawa wana nafasi kubwa sana ya kuwaathiri watoto wetu katika maisha mazima, tena athari hizi zinaweza kuendelea hadi utu uzima wao.
Achana na kupigwa au kuteswa kwa watoto wetu, hivyo angalau unaweza kuviona kwa macho, vipo vitu tele, tena vitu vibaya sana ambavyo huwezi kuviona wala kuvisikia, lakini vina athari kubwa sana kwa watoto wetu kutoka kwa wafanyakazi hawa.
Tujifunze kuishi nao vizuri, tujifunze kuwatia moyo na kuwapongeza pale wanapostahili, kama tunaweza kuwakaripia na kuwagombeza wakikosea, kwa nini tushindwe kuwapongeza wakifanya vizuri? Au unasahau kwamba wao ni watu pia? Wana moyo, wana hisia, wanachoka, wanaumia na wanakasirika kama wewe pia? Waruhusu waone kuwa ninyi kama familia mnatambua mchango wa kile wanachofanya, na kwamba juhudi zao ni za maana sana katika familia yenu.
Ni vema tukafanya haya kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wadada hawa wakalipiza visasi vya chuki na hasira kwa watoto wetu, ukajikuta kwa jinsi unavyowagandamizia mizigo ya kazi, mizigo ya hasira, na chuki ndivyo jinsi ambavyo unazidi kuwaweka watoto wako wanaoshinda nao katika hatari kubwa zaidi.
Zaidi ya yote tumruhusu Mungu kuwa mlinzi mkuu kwa watoto wetu kwa sababu wenyewe hatuwezi hii kazi. Tuwe macho na makini kila wakati.