NAHODHA wa Yanga, Dickson Job amezungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, kuwashukuru mashabiki kwa sapoti yao, tangu msimu huu kuanza hadi kufanikiwa kuchukua ubingwa.
Job amesema wanatambua mchango wa mashabiki ni mkubwa,unawapa nguvu ya kujituma zaidi uwanjani.
“Bado tuna kibarua kingine mbele yetu,msichoke kutuunga mkono katika fainali ya Kombe la FA tutakapokwenda kucheza Zanzibar.
“Tunataka kuchukua taji la FA, hivyo kama mlivyotuunga mkono katika mechi za Ligi Kuu, tunaomba msichoke, imebakia sehemu ndogo.
Lakini kwa upande wa winga wa timu hiyo, Aziz Ki alikuwa na machache ya kusema “Asante sana Wanayanga kwa kuja leo, ili tusherehekee kwa pamoja.”
Job aliyasema hayo wakati msafara wa Paredi la Kibingwa la kutembeza Kombe la Ubingwa kufika makao makuu ya klabu na kupokewa na nyomi la mashabiki walioambana na wale waliosindikia taji hilo toka Kwa Mkapa.
Yanga imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa tatu mfululizo ikiwa bado ina mechi mkononi ambapo kwa sasa ina pointi 77 na imesaliwa na mechi moja itakayopigwa keshokutwa jijini Dar es Salaam dhidi ya Tanzania Prisons.
KELELE ZAMPANDISHA BACCA JUKWAANI
Baada ya Rais wa Yanga, Injinia Said Hersi kumkaribisha kocha Miguel Gamondi, aseme neno kwa mashabiki, alipomaliza, mashabiki walianza kupiga kelele wakimtaka beki wao Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ampandishe jukwaani.
Hersi alilazimika kumpandisha Bacca jukwaani, jambo ambalo liliwafurahisha zaidi mashabiki hao.
Bacca ni mmoja ya nguzo imara ya Yanga katika safu ya ulinzi akishirikiana na Dickson Job, Yao Kouassi, Bakari Mwamnyeto, Joyce Lomalisa, Gift Fred, Kibwana Shomari na Nickson Kibabage.
Ukuta huo wa Yanga ndio kinara kwa kuruhusu mabao machache katika Ligi Kuu Bara msimu huu ambao Yanga wamebeba taji kwa msimu wa tatu mfululizo na kufikisha taji la 30 tangu ligi ilipoasisiwa mwaka 1965 ikiwa imefungwa 13 tu katika mechi 29, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 67 ikiwa pia ndo kinara.