Kipa Mnigeria ampa tuzo Aziz Ki

KIPA wa Tabora United, John Noble ameshindwa kujizuia na kuweka bayana kwa mtazamo wake Kiungo Bora kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara ni Stephane Aziz KI na kutoa sababu za kumpa tuzo nyota huyo wa Yanga anayeongoza kwa mabao akilingana na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.

Kipa huyo aliyetunguliwa mara mbili msimu huu na kiungo mshambuliaji huyo katika mechi za Ligi Kuu Bara zilizochezwa mjini Tabora alipofungwa 1-0 na ile ya juzi iliyopigwa Kwa Mkapa alipokula mabao 3-0, amesema ubora na ujuzi aliouonyesha hadi sasa ndio kinachombeba nyota huyo raia wa Burkina Faso.

Noble, ambaye ni raia wa Nigeria, alimchambua Aziz Ki namna anavyofunga mabao yake kwa kutumia akili ya kushtukiza, akitolea mfano anavyofunga kwa mguu wa kushoto na wakati mwingine kama kipa anakuwa anadhani anatoa pasi kwa mtu.

“Ukiachana na mabao 18 aliyonayo Aziz Ki, aina ya uchezaji wake wa kupiga mashuti, aina ya pasi zake anazotoa kwa wachezaji wenzake, nidhamu yake uwanjani ni kubwa si mchezaji ambaye ni mgovi,” amesema Noble na kuongeza;

“Sina maana viungo wengine ni wabaya, ila kwa upande wangu, aliye bora zaidi msimu huu ni Aziz Ki na anastahili kabisa kubeba tuzo. Mbali na yeye, kwa upande wa kipa aliyenivutia zaidi Djigui Diarra wa Yanga, kwani amefanya makubwa na kutumia ujuzi mkubwa awapo uwanjani.”

“Diarra ni kipa wa kisasa kwa maana ana uwezo wa kuanzisha mashambulizi, kuipanga timu, anajiamini kiasi kwamba anawasaidia mabeki wake kufanya kazi bila presha na mtazamo wangu Yanga imestahili kuchukua ubingwa kwa msimu huu kwa aina ya kikosi chake walichonacho,” ameongeza Noble.

Kuhusu Diarra amesema kuna wakati alimfuata na kumpa ushauri na kufichua; “Aliniambia mimi ni kipa mzuri, niendelee kupamba, hakuna mtu aliyewahi kuwa bora kwa siku moja, ubora unajengwa kutokana na mwendelezo wa kujituma.”

Diarra ndiye aliyekuwa Kipa Bora kwa misimu miwili mfululizo iliyopita, huku kwa msimu huu akiwa anachuana na Mkongoman, Ley Matampi wa Coastal Union kila mmoja akiwa na clean sheet 14 wakati Ligi Kuu ikimalizika kesho Jumanne.

Related Posts