NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Rajab Abdul ‘Harmonize’ a.k.a Konde Boy au Jeshi amewapagawisha mashabiki kwa kuwaimba vionjo vya baadhio ya nyimbo zake kisha kumpandisha jukwaani Stephane Aziz Ki mbele ya mashabiki katika Makao Makuu ya klabu hiyo, eneo la Jangwani.
Mara baada ya Konde kupanda jukwaani aliwachizisha wanayanga kwa kuimba kionjo cha wimbo wake wa Sijalewa, kisha alimuita Aziz Ki na kumuuliza maswali machache.
Msanii huyo alimwambia Aziz Ki awaahidi mashabiki wa Yanga kama ataendelea kusalia katika klabu hiyo kwa muda wa miaka mitatu, ndipo mchezaji huyo alinyoosha vidole viwili juu.
Baada ya Aziz Ki kunyosha vidole viwili juu, mashabiki hao wameshangilia kwa furaha, kisha mchezaji huyo mwenye mabao 18 katika Ligi Kuu Bara akilingana na nyota wa zamani wa klabu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyepo Azam kwa sasa anarudi sehemu ambayo alikuwepo.
Mara baada ya Aziz kwenda kukaa, Konde Boy hakuishia hapo, alitoa ahadi kwa mashabiki endapo timu hiyo ikifungwa hata mechi moja wakachome nyumbani yake moto, wapo walioshangalia na wengine kuguna.
Katika ligi ya msimu huu Yanga imepoteza mechi mbili ikifungwa na Ihefu na Azam kila moja kwa mabao 2-1, huku yenyewe ikishinda jumla ya mechi 25 na mbili nyingine ikitoka sare dhidi ya JKT Tanzania na Kagera Sugar na kuifanya itetee taji kwa msimu wa tatu mfululizo mapema ikiwa na mechi tatu mkononi pale ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1 na keshokutwa Jumanne itafunga msimu kwa kucheza na TZ Prisons.