Mamia ya waumini wajitokeza kuwekwa wakfu Askofu Mwasekaga

Mbeya. Mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki kutoka maeneo mbalimbali nchini wamejitokeza katika ibada maalumu ya kuwekwa wakfu, Askofu msaidizi mteule, Godfrey Mwasekaga.

Tukio hilo linafanyika leo JumapiliMei 26, 2024 katika Viwanja vya Sokoine jijini Mbeya huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa  mgeni rasmi katika ibada hiyo ya kumsimika kiongozi huyo wa kiroho.

Mwasekaga aliteuliwa na Papa Francis Machi 9, 2024 kabla ya wadhfa huo, alikuwa padri katika Parokia ya Mwanjelwa jijini Mbeya.

Pia, alikuwa Msaidizi wa Askofu Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu nchini (TEC).

Ibada ya kuwekewa wakfu huo, imeongozwa na Kardinali mstaafu Polycarp Pengo na maaskofu wengine akiwamo Askofu wa Jimbo Kuu la Mbeya na Rais wa TEC, Nyaisonga.

Tukio la kuwekewa wakfu kiongozi huyo, limeambatana na Jubilei ya miaka 125 ya uinjilisti huku ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Majaliwa ambaye ni mgeni rasmi.

Akizungumza katika ibada hiyo, Kardinali Pengo amemuomba askofu huyo kuwahudumia waamini wote wakiwamo masikini, wasafiri, wageni na makanisa yote.

“Usiache kushughulika na makanisa yote kwani wanahitaji msaada wako, kila mmoja ahakikishe injili inafundishwa kwani kutofanya hivyo ni kukiuka maelekezo ya Yesu,” amesema Kardinali Pengo.

Askofu msaidizi mteule, Mwasekaga alizaliwa Machi 7, 1976 huko Kyela, Mbeya. Amesoma katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino Peramiho, Jimbo Kuu Katoliki la Songea na hatimaye akapewa daraja takatifu ya upadri Julai 14, 2005 kwa ajili ya jimbo kuu la Mbeya.

Tangu wakati huo, aliteuliwa kuwa Paroko-usu wa Parokia ya Mtakatifu Claver, Mlowo kati ya mwaka 2005 hadi 2008. 

Amekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo na Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi kati ya mwaka 2006 hadi 2008.

Baadaye alitumwa na Jimbo Kuu la Mbeya kujiendeleza kwa masomo katika Taalimungu katika Taasisi ya Salesiano San Tommaso Messina nchini Italia. Alizama zaidi katika Taalimungu na kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Taalimungu kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian, kilichoko Roma kati ya mwaka 2008 hadi 2017.

Baada ya masomo yake, alirejea jimboni Mbeya na kuteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Claver, Mlowo kati ya mwaka 2018 – 2019. Kuanzia mwaka 2017 alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Katekesi Jimbo Kuu la Mbeya, Mkurugenzi wa Kituo cha Katekesi na Mratibu wa Liturujia ya Kanisa.

Kuanzia mwaka 2019, aliteuliwa kuwa ni Makamu Askofu Jimbo Kuu la Mbeya na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi iliyopo Mwanjelwa, Jimbo Kuu la Mbeya.

Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii ya Mwananchi kwa taarifa zaidi.

Related Posts