Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Beatrice Elias (36), mkazi wa Mtaa wa Katanini Wilaya ya Moshi kwa tuhuma za kumuua mumewe, Ephagro Msele (43) kwa madai ya kumkuta kwa mzazi mwenzake.
Kwa mujibu wa watu wa karibu na Msele, Mei 25, 2024, Beatrice baada ya kutoka msibani alikokuwa na mumewe, alimfuatilia kila anapokwenda kwa kutumia usafiri wa bodaboda na baada ya mumewe kuegesha gari lake mahali, alidaiwa kwenda nyumbani kwa mwanamke aliyezaa naye.
Inadaiwa kuwa, Beatrice alipofika nyumbani kwa mwanamke huyo, Kitongoji cha Pumuani A, alijificha getini na baadaye aligonga geti na mumewe ndiye aliyetoka kumfungulia.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa baada ya kukutana getini, yaliibuka mabishano kati yao, ndipo Beatrice alipofanikiwa kutekeleza tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amedai leo Jumapili Mei 26 kuwa, Beatrice alimvizia mumewe akitoka nyumbani kwa mzazi mwenzake na kumchoma na kitu chenye ncha kali.
“Ni kweli kumetokea hili tukio, usiku wa Mei 25, 2024 saa 3:50 usiku katika Kitongoji cha Pumuani A, Kata ya Kirua Vunjo, mtu aliyejulikana kwa jina la Ephagro Msele, mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Katanini, Kata ya Karanga, aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya mgongoni,” amesema Kamanda Maigwa.
Amesema wanamshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi na kwamba mwili wa mwanamume huyo umehifadhiwa Hospitali ya KCMC kwa hatua zaidi za kiuchunguzi.
“Wito wangu kwa wananchi waache kujichukulia sheria mkononi, taratibu zipo, watu wanaweza kukaa na kusuluhishana, maana madhara ni makubwa, tunakemea jambo hili,” amesema kamanda.
Akisimulia tukio hilo lilivyotokea, kaka wa marehemu, Peter Msele amesema mdogo wake alikuwa msibani jana, yeye na mkewe, baadaye alitoka kwenda kumfuata mwanamke aliyekuwa amezaa naye.
Amesema baada ya mkewe kujua kwamba mumewe anakwenda kwa mzazi mwenzake, alimfuata kimya kimya hadi nyumbani kwa mwanamke huyo.
“Jana mdogo wangu alikuwa kwenye msiba na mke wake, sasa baada ya kuzika akaondoka na kumuacha mke wake pale msibani na wakati huo, alikuwa amemfuata mwanamke ambaye amezaa naye huko Pumuani.
“Sasa mke wake akawa anamfuatilia, ikafika mahali akaacha gari njiani akapanda bodaboda kumfuata mume wake na huyu mama ni kama anapajua kwa huyo mwanamke aliyezaa na mume wake,” amesimulia ndugu huyo wa marehemu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Pumuani A, Abrahaman Mnyanyembe amesema baada ya kupigiwa simu kuwa kuna tukio la mauaji kwenye eneo lake, alifika haraka na kukuta mauaji hayo yamefanyika.
“Nilipigiwa simu jana usiku na wananchi wangu kuwa kuna tukio limetokea, kuna mtu anavuja damu nyingi kama kapigwa na chuma, niliamka haraka kwenda na kweli nilipofika eneo la tukio nilimkuta yule baba kalala chini na damu nyingi zinavuja.
“Niliwapigia simu polisi, wakafika eneo la tukio na wakati huo huyu mke wake (mtuhumiwa) yupo eneo la tukio, polisi walikagua na wakati wanachunguza mwili wa marehemu walikuta amechomwa kisu,” amedai Mnyanyembe.
Amedai kuwa wakati polisi wanatafuta kisu kilichotumika kumuua marehemu, kilikutwa kimefichwa kwenye pochi ya Beatrice pamoja na vitu vingine vya marehemu.
“Wakati tunatafuta kisu, bahati nzuri mke wa marehemu, aliwapa ndugu zake mkoba wake (pochi) ambao aliweka kisu kilichotumika kumuulia mume wake, simu zake pamoja na waleti ya mwanamume, vilikutwa kwenye ile pochi,” amedai mwenyekiti huyo.
Ameongeza kuwa mwanamke huyo ni kama aliweka doria nyumbani kwa huyo mwanamke mwingine (mzazi mwenzake Msele), kwamba mwanamume akiingia tu aambiwe.