MTU WA MPIRA: Azam FC inakuja taratibu, ubingwa haupo mbali

NANI anafuatilia maendeleo ya Azam FC? Najua sio watu wengi. Ni wachache sana.

Kwanini? Kwa sababu sio timu inayopendwa sana. Mashabiki wengi wa soka nchini wanazipenda Simba na Yanga. Ndizo timu za mioyo yao.

Azam ilivyoingia kwenye ligi kwa kishindo mashabiki wachache waliipenda. Wengine waliona ni kama timu yenye fedha imekuja kuzinyanyasa Simba na Yanga.

Kishindo chake cha kwanza kwenye ligi ilikuwa kumsajili Mrisho Ngassa kutoka Yanga. Yule Ngasa wa moto. Alikuwa ndiye mchezaji bora nchini kwa wakati ule. Ila kwa jeuri ya fedha Azam walimnunua na akacheza kwa mafanikio makubwa pale Chamazi.

Ndivyo hadithi ya Azam ilipoanzia. Mengine yaliyofuata yakawa historia.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliweka matarajio makubwa sana kwa Azam. Waliamini ni timu ambayo inakuja kumaliza utawala wa Simba na Yanga katika soka la Tanzania.

Lakini nini kimetokea? Bado wanajitafuta. Ni Miaka 10 sasa tangu Azam itwae ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Ilifanya hivyo msimu wa 2013-2014. Tukajua ni mwanzo wa timu hiyo kubeba makombe.

Lakini hadi leo miaka 10 baadaye hakuna hadithi mpya. Azam bado haijaweza kutwaa ubingwa mwingine wa ligi hiyo. Ushindani iliokuwa nao katika miaka ya mwanzo umepungua.

Pamoja na yote kuna kitu nimeanza kukiona tena kwa Azam. Imerudi kwenye ushindani.

Msimu huu Azam ilikuwa katika mbio za ubingwa hadi raundi ya 27. Imekuwa na ushindani tena. Ni mara ya kwanza baada ya misimu mingi.

Hadi sasa Azam ipo katika ushindani wa nafasi ya pili na Simba. Huenda wakamaliza juu ya Simba kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.

Wanaweka rekodi mpya kwenye Ligi. Hadi wanafungwa na Simba walikuwa wamecheza mechi 18 bila kapoteza. Ni rekodi nzuri.

Kwenye Kombe la Shirikisho (FA) wapo fainali. Huenda msimu huu wakafanya jambo na kubeba ubingwa wa FA ambao walishinda kwa mara ya kwanza mwaka 2019.

Nini kimebadilika kwa Azam? Nitakwambia baadhi ya vitu vichache.

Kwanza, msimu huu Azam umefanya usajili mzuri. Wachezaji kama Gjibril Sillah, Feisal Salum, Yannick Bangala wapo kwenye kiwango bora.

Pili, Azam ilifanya juhudi kubwa kuhakikisha wachezaji wote bora wanaendelea kusalia. Ndio hawa kina Kipre Junior, James Akaminko na wengineo.

Muunganiko wa nyota waliosalia na wapya wameifanya timu kuwa imara zaidi. Azam ya msimu huu ni bora kuliko ya msimu uliopita. Kuna mwanga unaonekana mbele.

Tatu, wamefanya maboresho mazuri ya benchi la ufundi. Kumleta kocha Youssouf Dabo mapema kabla ya kuanza kwa msimu kulimpa fursa nzuri ya kusuka timu yake. Uzuri ni kwamba ana msaidizi mahiri pia, Bruno Ferry. Ni kocha mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika.

Kuna wakati msimu huu baadhi ya wachezaji wa Azam walilalamika kuwa Dabo ni mkali sana. Wakataka atimuliwe, lakini viongozi wakakataa. Wakawaambia wachezaji wasiompenda Dabo waondoke wao. Viongozi wakaweka msimamo ambao mpaka sasa umewalipa.

Kitu kingine ambacho Azam imefanya msimu huu ni kurudisha watu wote wenye nasaba na timu yao. Watu waliokuwepo wakati wanapata mafanikio. Hii imewasaidia.

Wamerudisha zile posho za ushindi kama walivyokuwa wakifanya miaka ya nyuma. Wachezaji sasa wanajituma zaidi na ndio sababu msimu huu Azam imepoteza mechi tatu tu.

Kwa mwenendo huu wa Azam hadi sasa naona ikileta ushindani mkubwa zaidi msimu ujao.

Naona wameanza usajili mapema. Tayari wamesajili beki wa kati wa kurithi mikoba ya Daniel Amoah ambaye huenda akaondoka. Tayari wamesajili kiungo wa kuongeza nguvu katikati kwa kina Akaminko.

Nasikia pia wamesajili mastraika wawili kuziba nafasi ya Prince Dube. Hii ni ishara kuwa wanakwenda kushindana msimu ujao.

Naona kabisa kwa mwenendo wa Azam kwa sasa hawako mbali na kutwaa taji jingine la Ligi Kuu Bara.

Related Posts