Dar es Salaam. Waziri wa Mipango na Uwekezaji nchini Tanzania, Profesa Kitila Mkumbo amezitaka kampuni zinazotaka kuwekeza nchini kutilia mkazo maeneo ya vijijini, akibainisha idadi kubwa ya Watanzania wanaishi katika maeneo hayo.
Profesa Mkumbo amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa Kampuni ya Craft Silicon nchini Tanzania, inayotoa huduma za miamala ya fedha kwa njia ya kidigitali.
Amesema umuhimu wa mwelekeo wa idadi ya watu uliobainishwa na Sensa ya Watu na Makazi ya 2022:”Zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanaishi vijijini. Maeneo ya vijijini yana fursa kubwa za maendeleo na ustawi.”
“Kuwekeza katika maeneo haya sio tu kunawanufaisha wakazi wa maeneo hayo bali pia kunaleta manufaa kwa uchumi wa Taifa letu na kwa makampuni yenu pia. Inaongeza ubora wa maisha kwa mamilioni ya Watanzania.”
Waziri huyo amesema kutilia mkazo maeneo ya vijijini, kampuni zinaweza kusaidia kupunguza pengo kati ya mijini na vijijini, kuhakikisha kwamba faida za maendeleo ya kiuchumi zinawafikia Watanzania wote.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Craft Silicon, Kamal Budhabhatti amesema:”Kwa uwepo wetu wa ndani na utaalamu, tupo katika nafasi nzuri ya kusaidia ukuaji na maendeleo ya mfumo wa fintech wa Tanzania, kuwawezesha wafanyabiashara na kuendesha ustawi wa kiuchumi katika kanda hii.”
Amesema Craft Silicon inatazamia kushirikiana na biashara za ndani na taasisi za kifedha ili kuendeleza ubunifu wa fintech na kuwawezesha wafanyabiashara kustawi katika zama za kidigitali.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Mili Rughani amesema dhamira ya Craft Silicon katika soko la Tanzania inaenda zaidi ya kuanzisha ofisi ya ndani. Kampuni hiyo imejitolea kutumia rasilimali za ndani na kukuza mipango ya ujenzi wa uwezo ili kusaidia ukuaji na maendeleo ya mfumo wa fintech wa ndani.
“Kwa kuwawezesha vipaji vya ndani na kuwekeza katika maendeleo ya ujuzi, tunalenga kuendesha ukuaji endelevu wa kiuchumi na ubunifu nchini Tanzania,” amesema.